Chama cha SPD na uteuzi wa mgombea ukansela
24 Machi 2008Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni yaliyotangazwa siku ya Jumapili ,kiasi ya asilimia 91 ya wanachama wa SPD wanataka kupiga kura wenyewe kumchagua kiongozi atakaekuja kugombea wadhifa wa ukansela hapo mwakani.
Wakati huo huo makamu wa mwenyekiti wa chama hicho,Frank-Walter Steinmeier ambae pia ni Waziri wa Masuala ya Nje wa Ujerumani anasema,kabla ya kuanzisha midahalo ya kumteua mgombea wao,chama kinapaswa kueleza waziwazi mkondo wa kisiasa unaofuatwa na chama hicho.Amesema,chama hakina budi isipokuwa kudhihirisha kuwa ni chama kinachofuata sera za kati.Steinmeier anapinga kabisa kushirikiana na chama cha mrengo wa shoto Die Linke.Amesema kuwa baada ya uchaguzi mkuu utakaofanywa mwaka 2009,chama cha SPD hakitojaribu cho chote pamoja na Die Linke. Akasisitiza kuwa huo ni msimamo wa SPD na vivle vile ni msimamo wake binafsi.
Wakati huo huo kiongozi wa SPD,Kurt Beck amesema, atakapompendekeza mgombea ukansela,atazingatia mafanikio ya chama hicho.Akaongezea kuwa kiongozi atakaetoa changamoto kwa Kansela Angela Merkel katika uchaguzi wa mwaka 2009,atahitaji kuwa na uzoefu wa kisiasa na uwezo wa kuongoza.Beck akaeleza kuwa uamuzi wake utatangazwa baadae mwaka huu au mapema mwakani.
Lakini kura ya maoni imedhihirisha kuwa kutoka jumla ya raia 1,000 waliohojiwa,asilimia 87 wamepinga kumuachilia Beck kumteua mgombea ukansela.Yeye ameungwa mkono na asilimia 5 tu.Kiongozi huyo wa SPD alipoteza sana umaarufu wake,baada ya kuashiria uwezekano wa kufanywa majadiliano pamoja na chama cha Die Linke kinachoelemea mrengo wa shoto,katika jeribio la kutaka kuunda serikali ya jimbo la Hesse.Lakini hivi karibuni alisema ,vyama vya SPD na Die Linke vina misimamo tofauti kuhusu masuala mengi kama vile katika siasa za nje,au sekta zinazohusika na fedha,jamii na uchumi. Amesema,tofauti hizo ni kubwa mno na kwa hivi sasa hakuna msingi wa kuweza kushirikiana kisiasa.
Licha ya kupoteza umaarufu wake miongoni mwa wanachama wa SPD,Kurt Beck amesema,yeye hafikirii kujiuzulu na kamwe hajuti kushika wadhifa wa mwenyekiti wa chama.Akaongezea kuwa mtu hakimbii shida,matatizo yanapoibuka.