1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump azidi kushinikizwa kumlaani mwanamfalme wa Saudia

5 Desemba 2018

Maseneta wa Marekani wamesema wameridhika bila chembe ya shaka kwamba mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman alihusika katika mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/39UUQ
G20-Gipfel in Buenos Aires | USMCA-Abkommen | Donald Trump, Präsident USA
Picha: Reuters/K. Lamarque

Katika kile kinachoonekana kama kujitenga na Rais Donald Trump, maseneta hao wametoa kauli hiyo baada ya kufanya mkutano na Mkurugenzi wa Ujasusi wa Marekani CIA Gina Haspel. Mtazamo huo wa maseneta unamuongezea shinikizo Rais Trump kumlaani hadharani Bin Salman.

Seneta Lindsey Graham wa chama cha Republican aliyeitisha mkutano huo na Haspel, amesema haiwezekani kwamba mwanamfalme huyo hakuhusika katika kifo cha Khashoggi. Seneta huyo ameongeza kuwa ambaye hakubali kuwa mauaji hayo yalipangwa na watu walio chini ya amri ya mwanamfalme huyo basi atakuwa ni kama mtu aliye na "upofu wa kujitakia."

Anayekataa Bin Salman alihusika basi ni "kipofu wa kujitakia"

Mwenyekiti wa masuala ya mambo ya nje wa seneti Bob Corker pia kutoka chama cha Republican cha Rais Trump, amesema anaamini iwapo mwanamfalme huyo angefunguliwa mashtaka, majaji wangemkuta na hatia katika kipindi cha nusu saa tu.

USA Washington Senator Bob Corker
Seneta Bob Corker wa chama cha Republican akizungumza na waandishi wa habariPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Walsh

"Sina shaka yoyote akilini mwangu kwamba mwanamfalme Mohammed Bin Salman aliamrisha na kusimamia mauaji hayo, alijua kabisa kilichokuwa kinaendelea na alipanga mapema," alisema Corker. "Kama angekuwa mbele ya jopo la majaji, angepatikana na hatia baada ya dakika thelathini tu. Kwa hiyo swali ni, tufanyeje kuhusiana na suala hilo? Kwa sasa ni bahati mbaya lakini nafikiri wanahisi kana kwamba jambo hili limetokea na likapita tu," aliongeza seneta huyo.

Kauli hizi za wazi kabisa za wanachama wa chama cha Rais Donald Trump mwenyewe unakinzana na inachosema ikulu ya White House, inayokataa kuwepo na uhusiano wa moja kwa moja kati ya mwanamfalme Mohammed Bin Salman na kuuwawa kwa mwandishi na mkosoaji wa uongozi wa Saudia, Khashoggi, katika ubalozi wa nchi hiyo huko Uturuki.

Trump alionya mahusiano ya Marekani na Saudia hayawezi kuharibiwa

Trump amekuwa akitumia kauli za kupotosha kuhusiana na mtu wa kulaumiwa kwa mauaji hayo, jambo lililowavunja moyo maseneta ambao kwa sasa wanatafuta njia za kuiadhibu Saudi Arabia, ambayo ni mshirika wa muda mrefu wa Marekani.

Saudi Arabien, Kronprinz - Mohammed bin Salman
Mwanamfalme wa Saudia Mohammed Bin SalmanPicha: Getty Images/F. Nureldine

Baada ya ripoti kwamba shirika la ujasusi la Marekani, CIA, lilihitimisha katika uchunguzi wake kwamba mwanamfalme huyo aliamrisha kuuwawa kwa Khashoggi, Trump alionya kwamba mahusiano ya Marekani na Saudi Arabia pamoja na uthabiti wa soko la mafuta, ni mambo muhimu mno kuyavunja kutokana na sakata hiyo ya mauaji.

Khashoggi aliuwawa Oktoba 2. Mwandishi huyo wa habari aliyeishi marekani kwa muda na aliyekuwa analiandikia gazeti la Washington Post, alikuwa akiukosoa utawala wa Saudia. Aliuwawa ubalozini alipokuwa amekwenda kushughulikia nyaraka zake za ndoa katika kile ambacho maafisa wa Marekani wamekielezea kama njama iliyopangwa vizuri. 

Mwandishi: Jacob SafariAFPE/APE

Mhariri: Gakuba Daniel