1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

090409 Parlamentswahl Indonesien

Charo Josephat/ ZP/ Musch Borowski9 Aprili 2009

Uchaguzi wakumbwa na machafuko katika eneo la Papua

https://p.dw.com/p/HTyV
Rais wa Indonesia Susilo Bambang YudhoyonoPicha: AP

Chama cha Democratic cha siasa za mrengo wa kati nchini Indonesia kinakaribia kushinda uchaguzi wa bunge uliofanyika hii leo nchini humo. Kwa mujibu wa kura zilizohesabiwa, chama hicho cha rais Susilo Bambang Yudhoyono wa Indonesia kinaongoza mbele ya chama cha kizalendo cha Democratic Party of Struggle, PDI-P cha rais wa zamani, Megawati Sukarnoputri. Uchaguzi huo umekumbwa na machafuko katika eneo la Papua.

Watu watano wameuwawa katika eneo la Papua saa chache kabla upigaji kura kuanza, kwenye mfululizo wa mashambulio ambayo waasi waliojitenga wananyoshewa kidole kuhusika. Waasi hao wamekuwa wakipigana vita vya chini kwa chini tangu miaka ya 1960 kutaka uhuru wa eneo la Papua. Waziri wa ulinzi wa Indonesia, Widodo Adisucipto, ameyaeleza machafuko ya Papua kwamba juhudi ya makusudi kuhujumu uchaguzi wa leo na kuongeza kwamba maafisa takriban 100 zaidi wa polisi wametumwa katika eneo hilo kutuliza hali ya mambo na kushika doria.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yanayojumulisha kura kutoka kwa vituo mbalimbali vya kupigia kura zilizohesabiwa na taasisi ya utafiti nchini Indonesia, chama cha rais Susilo Bambang Yudhoyono, kinaongoza kwa asilimia 20.8 ya kura zote zilizopigwa. Mkurugenzi wa taasisi hiyo Saiful Mujani, amesema kuna haja ya kusubiri kuona ni chama kipi kitakachochukua nafasi ya pili na ya tatu.

Matokeo hayo ambayo si rasmi yanalingana na kura za maoni za hapo kabla ambazo zimebashiri kwamba chama cha Democratic kitashinda uchaguzi wa bunge baada ya kushika nafasi ya tano katika uchaguzi wa mwaka 2004. Rais Yudhoyono mwenyewe ndiye anayepigiwa upatu kushinda uchaguzi wa rais mwezi Julai mwaka huu, huku umaarufu wake ukiwa zaidi ya asilimia 60 nchini Indonesia.

Ex Diktator Suharto ist tot
Rais wa zamani wa Indonesian SuhartoPicha: AP

Usumbufu katika kupiga kura

Uchaguzi wa leo ni wa tatu wa bunge tangu kung´olewa madarakani kwa kiongozi wa kiimla wa Indonesia, Suharto, zaidi ya muongo mmoja uliopita, hatua ambayo ilikaribisha enzi ya mageuzi ya kidemokrasia nchini humo. Kwa mara ya kwanza katika mwaka huu wabunge wamechaguliwa moja kwa moja badala ya kupitia orodha ya vyama. Makaratasi ya kupigia kura yalikuwa makubwa safari hii kama picha ya gazetini. Kwa wapigaji kura wengi haikuwa kazi rahisi.

"Nilichanganyikiwa kidogo. Katika uchaguzi uliopita tulilazimika kutundika majina wa wagombea kwenye makarati ya uchaguzi na safari hii kuweka alama kwenye jina la mgombea unayemtaka. Na karatasi la kupigia kura lilikuwa kubwa zaidi safari hii kuliko uchaguzi uliopita."

Kama sehemu ya mageuzi ya sheria za uchaguzi, kwa mara ya kwanza wapigaji kura walitakiwa kuweka alama kwenye karati ya kura kumchagua mgombea au chama au vyote viwili. Makamu wa rais wa Indonesia, Jusufu Kalla, amekiri kwamba haikuwa rahisi kupiga kura leo. "Hata sisi tunaoelewa imetuwia vigumu, sembuse watu ambao hawajui kusoma na kuandika," amesema kiongozi huyo baada ya kupiga kura kwenye kituo kilicho karibu na nyumbani kwake mjini Jakarta.

Wapigaji kura zaidi ya milioni 171 katika taifa lenye watu takriban milioni 230 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa leo. Viti 18,560 katika mabunge ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya vinashindaniwa. Vile vile kuna viti 132 katika baraza la wawakilishi. Vyama 38 vimeshiriki kwenye uchaguzi huo, na sita kati yao vinashindania viti katika mabaraza ya mkoa na wilaya katika jimbo la Aceh. Vyama sita pekee vinatarajiwa kushinda viti katika baraza la wawakilishi.

Nur anasema amepiga kura lakini hawajui wagombea aliowapigia kura kwa kuwa ni wengi mno. "Mpaka sasa siwafahamu wagombea ni akina nani. Nimeweka alama tu kwenye nembo ya chama. Ninatumai mambo yatakuwa mazuri nchini Indonesia baada ya uchaguzi huu."

Matokeo ya mwisho rasmi ya uchaguzi wa leo yanasubiriwa kutolewa mwezi ujao wa Mei mwaka huu.

Mwandishi:Musch,Borowski/ZR/Josephat Charo

Mhariri:A.AbdulRahman.