Chama cha Merkel chafikia makubaliano katika majimbo mawili
14 Juni 2017Uchaguzi katika majimbo hayo unaweza kuwa dalili ya kile kinachoweza kutokea katika uchaguzi mkuu mwezi Septemba , ambapo Merkel anawania muhula wa nne madarakani.
Wiki nne baada ya kupata ushindi na wingi usiotarajiwa katika jimbo la North Rhine Westphalia, chama cha kansela wa Ujerumani Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU pamoja na chama kinachoelemea upande wa wafanyabiashara cha Free Democrats FDP vimefikia makubaliano kuunda serikali katika jimbo hilo lenye wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani.
"Makubaliano ya kuunga muungano yamekamilika" amesema mwenyekiti wa jimbo wa chama cha CDU Armin Laschet baada ya duru ya saba ya majadiliano katika muda wa wiki tatu. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwekwa wazi siku ya Ijumaa.
Kubwa miongoni mwa makubaliano kadhaa ni mtazamo wa "kutovulimia kabisa" katika suala la usalama. Mipango hiyo inajumuisha upanuzi wa uchunguzi kupitia kamera za vidio pamoja na jeshi la polisi.
"Bado tuna kazi ya kufanya , lakini masuala makuu muhimu yamekwisha tatuliwa," amesema kiongozi wa chama cha FDP Christian Lindner. baina yao , vyama hivyo viwili vina viti 100 kati ya viti 199 katika bunge la jimbo hilo , Landtag.
Laschet atawania kuchaguliwa kuwa waziri mkuu wa jimbo Juni 27 katika bunge , Landtag, mrithi wa Hannelore Kraft kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto Social Democrats , SPD.
Muungano pamoja na chama cha kijani
Katika jimbo la Schleswig-Holstein , jimbo lililoko kaskazini kabisa mwa Ujerumani , chama cha CDU na FDP vinaelekea katika kuunda serikali pamoja na chama cha Kijani.
"Tumekuwa na mazungumzo magumu," kiongozi wa jimbo la chama cha CDU Daniel Günther alisema baada ya mazungumzo ya kuunda serikali, licha ya kuwa majadiliano yamekuwa yakifanyika " katika hali nzuri ya maelewano."
Mkuu wa majadiliano wa chama cha walinzi wa mazingira , chama cha kijani , Monika Heinold, amesema makubaliano yamekuwa na kile alichokiita "alama za walinzi wa mazingira." Kiongozi wa FDP Heiner Garg wakati huo huo alisema vyama hivyo vimefanikiwa katika kuweka muongozo wa "maono ya baadaye kwa ajili ya jimbo hilo la Schleswig-Holstein." Msemaji wa chama cha FDP amethibitisha kwamba makubaliano yamefikiwa , lakini hakutoa maelezo zaidi.
Kama ilivyokuwa katika jimbo la North Rhine Westphalia , chama cha CDU kiliiondoa serikali iliyokuwapo ambayo ilikuwa inaongozwa na chama cha SPD na ikijumuisha chama cha kijani.
Merkel anawania muhula wa nne madarakani, amekuwa akiongoza serikali ya mseto tangu mwaka 2013 pamoja na chama cha Social Democrats katika kiwango cha serikali kuu ya shirikisho. Chama cha Christian Democratic na Free Democrats viliongoza serikali ya Ujerumani kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2013.
Uchunguzi wa maoni kwa hivi sasa unakipa chama cha kihafidhina uongozi katika kiwango cha kitaifa kabla ya uchaguzi wa mwezi Septemba, ambapo mgombea wa chama cha SPD Martin Schulz akipungua kasi baada ya kupata uungwaji mkono mkubwa mwanzoni.
Mwandishi: Sekione Kitojo /
Mhariri: Yusuf , Saumu