1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha MDC chaongoza katika viti vya ubunge Zimbabwe.

1 Aprili 2008
https://p.dw.com/p/DYqn

Harare.

Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe imetoa matokeo ya majimbo 132 ya uchaguzi wa bunge hadi sasa na kusema kuwa chama cha upinzani cha MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai kimepata viti 68 dhidi ya 64 vya chama tawala cha ZANU-PF.

Matokeo rasmi ya kura za urais bado hayajatangazwa. Chama cha upinzani cha MDC kinadai kuwa kiongozi wao Morgan Tsvangirai amepata asilimia 60 ya kura za urais dhidi ya asilimia 30 ya rais Mugabe.

Madai hayo ya chama cha upinzani yanatokana na jumla ya kura walizojumlisha kutokana na matokeo yanayowekwa katika vituo vya kupigia kura. Hata hivyo matokeo ya hivi sasa yanaonyesha kuwa uchaguzi wa duru ya pili hauwezi kuepukika kati ya kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai na rais Robert Mugabe.

Matokeo yameendelea kupatikana kwa taratibu mno na chama cha MDC kimeishutumu tume ya uchaguzi kuchelewesha kwa maksudi matokeo katika juhudi za kutaka kufanya udanganyifu na kumpendelea Mugabe.Maafisa wa tume ya uchaguzi wamewataka Wazimbabwe kuwa wenye subira wakati matokeo hayo yanatangazwa. Kuhusiana na njama za kutaka kufanya udanganyifu , rais Mugabe amepuuzia madai hayo akisema kuwa huo ni uzushi wa mataifa ya magharibi.

Wakati huo huo , mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Paris wameitaka tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe kutangaza matokeo haraka kwa kuwa wanasubiri kwa hamu kufanyakazi na maafisa waliochaguliwa kidemokrasia nchini Zimbabwe.