Chama cha mazingira champa kisogo Merkel
16 Oktoba 2013Akizungumza na waandishi wa habari baada kushindwa kwa mazungumzo kati ya chama chake na chama cha Christian Democratic, CDU, cha Angela Merkel, mwenyekiti wa chama cha walinzi wa mazingira Claudia Roth alieleza bayana kuhusu hatua inayofuata. ''Chama cha walinzi wa mazingira hakitaki tena kuzungumza juu ya kuundwa kwa serikali ya mseto'', alisema mwenyekiti huyo.
Viongozi wa chama cha walinzi wa mazingira na wenzao wa muungano wa kihafidhina unaoongozwa na Angela Merkel, waliyataja mazungumzo yaliyokwama kati yao kuwa ya wazi na mazito.
''Mazungumzo yamekuwa marefu, na magumu. Badala ya kuzungukazunguka, yametuwama kwenye masuala muhimu. Hata hivyo, tumeamua kwamba katika mkutano wetu wa chama, hatutalijadili suala la kuunda serikali ya mseto.'' Alisema Claudia Roth.
Pengo kubwa kimtazamo
Hata hivyo pande hizo mbili zilishindwa kupata maridhiano juu ya masuala muhimu kama vile kodi kwa watu wenye kipato kikubwa, mageuzi katika bima ya afya, na kiwango cha chini cha mshahara.
Licha ya hayo, katibu mkuu wa chama cha CDU, Hermann Gröhe, amesema mazungumzo kati yao na chama kinachotetea mazingira ambacho ni hasimu wao mkubwa, yalikuwa hatua nzuri. ''Nadhani mazungumzo yalikuwa na azma inayolenga mbali kupita siku za hivi karibuni; kila upande kusikiliza mwenzake na kujaribu kupata muafaka. Hiyo ni hatua nzuri kwa kazi tunayoifanya bungeni.'' Alisema.
Claudia Roth alisema haikuwepo haja ya kuingia katika mkondo wa tatu wa mazungumzo, kwa sababu baada ya mikutano miwili ambayo imeyajadili masuala yote kwa kina, hakuna upande ulioelekea kulegeza msimamo wake. Kwa kuzingatia hali hiyo, amesema Bi Roth, hakuna msingi imara kwa serikali ya mseto kati ya vyama hivyo.
Kukubali kutokubaliana
Kwa upande wake katibu mkuu wa chama cha CDU, Hermann Gröhe, amesema anaamini pengo lililopo katika mitazamo ya vyama hivyo linaweza kuzibwa. ''Nataka kusisitiza kuwa pamoja na tofauti za kimtazamo, hakukuwa na kipengele katika mazungumzo ambacho tumekiona kama kitu kisichowezekana kabisa'', amesema Gröhe.
Baada ya kupewa kisogo na chama cha walinzi wa mazingira, Bi Merkel sasa anabaki na chaguo moja tu, nalo ni kujadiliana na chama kikuu cha upinzani, SPD. Haitakuwa mara ya kwanza kwa vyama hivyo kuwa katika serikali ya mseto, kwani vilifanya hivyo katika muhula wa kwanza wa Angela Merkel.
Kura ya maoni ya umma iliyofanywa hivi karibuni, imeonyesha kuwa wajerumani wengi wanapendelea serikali ya mseto kati ya vyama hivyo vikubwa. Bi Merkel amekuwa akiwasaka washirika wa kuunda serikali ya mseto tangu Septemba 22, baada ya chama chake kushinda uchaguzi mkuu, lakini kikiwa na upungufu wa viti 5 bungeni kuweza kuunda serikali peke yake.
Mwandishi: Daniel Gakuba/DW English Website
Mhariri: Josephat Charo