Chama cha Imran Khan chaitisha maandamano ya nchi nzima
4 Novemba 2022Chama hicho Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI), kimeitisha maandamano ya nchi nzima Ijumaa, mnamo wakati hali ya taharuki ikiendelea kutanda katika taifa hilo la kusini mwa bara Asia.
Asad Umar ambaye ni msaidizi wa karibu wa Khan ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba baada ya sala ya Ijumaa mchana, kutakuwa na maandamano kote nchini na maandamano hayo yataendelea hadi pale matakwa ya Khan yatakapoitikiwa.
Kando na kutaka uchaguzi wa mapema, chama cha Khan Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) - pia kinamtaka Waziri Mkuu Shehbaz Sharif kujiuzulu. Shehbaz aliongoza muungano wa kisiasa uliomuondoa Khan madarakani kupitia kura ya bunge mwezi Aprili.
Imran Khan alipigwa risasi mguuni jana alipokuwa juu ya lori akiongoza maandamano mjini Islamabad kushinikiza serikali kuandaa uchaguzi wa mapema.
Wafuasi wa Khan wajitokeza kwa maandamano Ijumaa
Khan azindua maandamano kushinikiza uchaguzi wa mapema Pakistan
Wafuasi wa Khan walianza kukusanyika mapema Ijumaa katika eneo ambalo Khan alipigwa risasi wakimtaka Khan aanzishe tena maandamano hayo mjini Islamabad.
"Maandamano sharti yaendelee. Hatuwezi kuyaacha. Watu wana hasira sana. Wakati huu yatakuwa makubwa Zaidi,” amesema Ansar Bashir, mfuasi wa Khan mwenye umri wa miaka 40 aliyekuwa karibu wakati Khan aliposhambuliwa. Aliliambia shirika la Habari la Reuters huku akibeba kijibendera cha chama cha Khan PTI.
Alisema alikuwa umbali wa takriban mita 30 kutoka mahali Khan alipigwa risasi. Polisi wamezingira eneo hilo na wamekuwa wakifanya upekuzi na uchunguzi usiku kucha wakikusanya ushahidi.
Polisi wachunguza nini ilichochea shambulizi
Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan afunguliwa mashitaka ya ugaidi
Polisi haijatoa kauli yoyote rasmi kuhusiana na shambulizi hilo. Lakini maafisa wake wamemtia mbaroni mshukiwa aliyefanya shambulizi hilo. Kanda ya video iliyonaswa wakati wa shambulizi hilo imeashiria mshambuliaji alichochewa na Imani ya kidini.
Alighadhabishwa na kauli za Khan kulinganisha juhudi zake za kisiasa na za Mtume wa Waislamu.
Khan alilazwa hospitalini mjini Lahore. Madaktari wanaomhudumia wamesema hayuko katika hali mahututi. Hata hivyo yeye mwenyewe pia hajazungumza hadharani kuhusu tukio hilo.
Waziri Mkuu na serikali yake yadaiwa kuhusika
Kulingana na msemaji wa serikali ya jimbo la Punjab ambaye pia ni mwanachama wa PTI Mussarat Jamshed Cheema, Khan ametaka uchunguzi ufanywe dhidi ya Waziri Mkuu Sharif, Waziri wa Mambo ya Ndani Rana Sanaullah na mkuu wa intelijensia Meja Jenerali Faisal, akiwatuhumu kuhusika na shambulizi hilo. Khan na chama chake hawajatoa Ushahidi wowote kuthibitisha madai yao.
Sharif na Sanaullah wamelaani shambulizi hilo lakini wamekana kuhusika. Jeshi halikutoa kauli lilipoulizwa kuzungumzia shambulizi la Khan, lakini hapo awali lililaani tukio hilo.
Sharif ametaka pia uchunguzi huru kufanywa kuhusu shambulizi lililofanyika katika eneo hilo wakati chama cha Khan kilikuwepo madarakani.
Khan aliingia madarakani mwaka 2018 baada ya uchaguzi mkuu uliogubikwa na madai ya udanganyifu uliofanywa na jeshi la nchi hiyo.
(RTRE; DPAE)
Tafsiri: John Juma