1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Freedom chashinda uchaguzi wa bunge Austria

Josephat Charo
30 Septemba 2024

Chama hicho kimenufaika kutokana na wapiga kura kukatishwa tamaa na mfumko mkubwa wa bei, vita nchini Ukraine, janga la COVID-19 pamoja na wasiwasi wao kuhusu uhamiaji.

https://p.dw.com/p/4lDUQ
Mkuu wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Freedom nchini Austria, Herbert Kickl
Mkuu wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Freedom nchini Austria, Herbert KicklPicha: Alex Halada/AFP/Getty Images

Chama cha mrengo mkali wa kulia nchini Austria, Freedom Party, kimepata ushindi wa kwanza wa kihistoria katika uchaguzi wa bunge la kitaifa uliofanyika jana Jumapili.

Chama hicho kimekamilisha mbele ya chama kinachotawala cha kihafidhina cha Conservative kikitumia wasiwasi uliokuwepo miongoni mwa wapiga kura kuhusu uhamiaji, mfumuko wa bei, vita vya Ukraine na masuala mengine muhimu.

Matokeo ya awali yanaonyesha chama cha Freedom kinashika nafasi ya kwanza kikijipatia asilimia 29.2 ya kura na chama cha kansela Karl Nehammer cha Austrian People's Party kikishika nafasi ya pili na asimilia 26.5 ya kura.

Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic kimeshika nafasi ya tatu na asilimia 21 ya kura. Serikali ya mseto inayoondoka ya chama cha Austrian People's Party na chama cha Kijani, Greens, imepoteza wingi wake katika baraza la chini la bunge.

Kiongozi wa chama cha Uhuru, Herbert Kickl, anataka kuwa kansela wa Austria na amesema yuko tayari kuzungumza na vyama vingine vya siasa kuunda serikali ya mseto.