1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CDU chashinda uchaguzi Schleswig-Holstein

Josephat Charo
9 Mei 2022

Chama cha kihafidhina cha Ujerumani cha Christian Democratic Union, CDU kimeshinda uchaguzi katika jimbo la kaskazini la Schleswig-Holstein.

https://p.dw.com/p/4B0ct
Landtagswahl Schleswig-Holstein | MP Günther CDU Wahlparty
Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

 Chama cha mbadala kwa Ujerumani AfD kimetupwa nje ya bunge la jimbo hilo, huku chama cha Social Democratic SPD kikifanya vibaya katika uchaguzi huo ambao umeonekana kama mtihani wa jinsi kansela Olaf Scholz anavyovishughulikia vita vya Ukraine. 

Waziri Mkuu mashuhuri wa jimbo la Schleswig-Holstein Daniel Günther wa chama cha CDU ameongoza mbele ya wagombea wa chama cha Kijani na chama cha Social Democratic, SPD na kuboresha kwa kiwango kikubwa matokeo yake ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

Chama cha SPD ambacho katika ngazi ya kitaifa kinaongoza serikali ya mseto, kansela Olaf Scholz akiwa katika usukani, kimeporomoka na kupata matokeo mabaya kabisa kuwahi kuyapata katika chaguzi za majimbo katika jimbo hilo na kumaliza nyuma ya chama cha Kijani, ambacho kimeshika nafasi ya pili kikishinda asilimia 18.3 ya kura.

Chama kinachopendelea biashara cha FDP kmejikusanyia asilimia 6.4 ya kura. Chama cha Social Democratic SPD kikiongozwa na mgombea wake Thomas Losse-Müller kimepata asilimia 16 ya kura, matokeo ambayo ni mabaya zaidi kuliko ya asilimia 25.4 ya uchaguzi wa wmaka 2009.

Chama cha mrengo wa kulia cha Mbadala cha Ujerumani AfD kimepata asilimia 4.4 na kimeshindwa kufikisha kiwango cha asilimia tano ya kura kinachotakiwa kuwa na uwakilishi bungeni na hivyo hakitarejea katika bunge la jimbo hilo mjini Kiel. Hii ni mara ya kwanza kwa chama cha AfD kutolewa nje ya bunge la jimbo la Ujerumani. Chama hicho kilikuwa na asilimia kati ya 5 na 6 katika kura za maoni. Mgombea wake Jörg Nobis amesema mivutano ya ndani bila shaka imewafanya wapiga kura kutokiunga mkono.

Günter kuunda serikali ya mseto atakavyo

Waziri Mkuu mashuhuri wa jimbo la Schleswig-Holstein Daniel Günther wa chama cha CDU sasa ana fursa kadhaa za kuunda serikali ya mseto. Anaweza kuendelea na serikali ya sasa ya mseto na chama cha Kijani na FDP, lakini sasa mseto wa vyama viwili unawezekana pia.

Schleswig Holstein Landtagswahl | CDU
Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Akizungmza mbele ya wafuasi waliokuwa wakishangilia ushindi, Günther alizungumzia kura kubwa ya imani na bila shaka kuungwa mkono kwake yeye binafsi akisema matokeo yanaonesha watu wameridhika na jinsi wanavyoongoza serikali.

"Na tulichotangaza wakati wa kampeni kuwa tuna fursa hata wakati huu mgumu kulipa nguvu mpya jimbo la Schleswig-Holstein, kuyafikia melengo ya ulinzi wa mazingira na kuvutia ajira nchini mwetu ndiho tutakachoendelea kukifuatilia katika miaka mitano ijayo, kufanya kazi kwa bidii ili kuthibitisha uhalali wa uaminifu huu tuliopewa, pia katika eneo hili."

Matokeo ya uchaguzi wa Jumapili ni ufanisi mkubwa wa kwanza kwa chama cha CDU katika kipindi cha karibu mwaka mmoja baada ya mfululizo wa kushindwa katika ngazi ya shirikisho na katika majimbo kadhaa, hivi karibuni kabisa katika uchaguzi wa jimbo la Salaand.

Uchaguzi wenye umuhimu mkubwa hata hivyo ni uchaguzi wa jimbo utakaofanyika Jumapili ijayo katika jimbo la North Rhine Westphalia, jimbo lenye idadi kubwa ya wakazi nchini Ujerumani, ambao mara kwa mara huelezwa kama "uchaguzi mdogo wa bunge la Ujerumani"

Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Hendrik Wüst alisherehekea ushindi wa chama cha CDU katika uchaguzi wa jimbo la Schleswig-Hoslstein akisema ni ishara nzuri kwa uchaguzi wa jimbo lake wiki ijayo. Kura za maoni hata hivyo zinaonesha mnyukano mkali kati ya chama cha CDU na SPD.

dpa