Chaguzi za magavana zitafanyika majimboni Nigeria
21 Aprili 2011Katika hotuba hiyo kwa taifa, Rais Goodluck Jonathan ametoa wito kwa wananchi kukomesha ghasia zilizosababisha umwagaji damu hasa katika kaskazni mwa nchi wanakoishi Waislamu wengi. Amesema na hapa ninamnukuu, "Machafuko hayo yanakumbusha matukio ya huzuni yaliyoitumbukiza nchi katika vita vya wenyewe kwa miezi 30. Ghasia hizi hazikuchochewa pekee kisiasa. Ni dhahiri kuwa lengo ni kufuja chaguzi zijazo - na hilo halikubaliki kabisa". Mwisho wa kumnukuu. Hapo Rais wa Nigeria alikuwa akikumbusha mgogoro wa miaka ya 1960 ambapo kiasi ya watu milioni moja waliuawa.
Machafuko haya mapya, yalizuka baada ya Goodluck Jonathan, Mkristo anaetokea kusini ya Nigeria kutangazwa mshindi, baada ya kujinyakulia asilimia 57 ya kura katika uchaguzi wa rais uliofanyika Jumamosi iliyopita. Mpinzani wake mkuu, Muhammadu Buhari, Muislamu kutoka kaskazini ya Nigeria, alipata asilimia 31 ya kura zilizopigwa. Vijana waliohamaki wakaanza kufanya ghasia katika miji ya kaskazini. Wafuasi hao wa Buhari wamepinga matokeo ya uchaguzi na katika ghasia hizo, makanisa, misikiti na nyumba zilitiwa moto. Serikali imekataa kutaja idadi ya watu waliouawa, ikihofia machafuko zaidi. Lakini makundi ya haki za binadamu ya Nigeria yanasema, zaidi ya watu 200 wameuawa. Na kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu, takriban watu 40,000 wamepoteza makaazi yao na wengi wao wanatafuta hifadhi katika vituo vya polisi na kambi za kijeshi.
Jonathan alishika madaraka mwezi wa Mei mwaka 2010, baada ya mtangulizi wake Umaru Yar'Adua, Muislamu kutoka kaskazini, kufariki dunia kabla ya kumaliza muhula wake wa kwanza. Hatua hiyo, ilisababisha chuki katika eneo la kaskazini lililopoteza nyadhifa hiyo. Licha ya ghasia zilizozuka kufuatia uchaguzi wa wiki iliyopita, wasimamizi wameusifu mchakato wa uchaguzi kama ni hatua ya kusonga mbele kwa Nigeria, mzalishaji mkubwa kabisa wa mafuta barani Afrika na yenye historia ya chaguzi za ghasia na udanganyifu. Hata hivyo, wanasema kuwa Nigeria bado ina matatizo makubwa. Kwani machafuko hayo mapya yamezusha wasiwasi iwapo nchi hiyo itaweza kuendelea na duru ya tatu na ya mwisho ya uchaguzi wa magavana na mabunge katika majimbo 36 hapo tarehe 26 Aprili. Lakini Rais Jonathan katika hotuba yake ameahidi kuwa chaguzi zitafanywa kama ilivyopangwa na vikosi vya usalama vitachukua hatua kama inavyohitajika kukabiliana na machafuko yo yote yatakayozuka.
Nigeria yenye wakaazi wengi kabisa barani Afrika ikiwa na watu milioni 150, imegawika sehemu mbili: kaskazini wanakoishi Waislamu wengi na kusini kwenye Wakristo wengi. Lakini serikali inasema, ghasia zilizozuka hazihusiki na dini wala ukabila, bali zimechochewa na wale wanaopinga matokeo ya uchaguzi wa Jumamosi iliyopita.
Mwandishi:MartinPrema/AFPE/RTRE
Mhariri:Josephat Charo