Chad: Hakuna mazungumzo na waasi waliomuua Deby
26 Aprili 2021Serikali ya mpito ya kijeshi nchini Chad imesema haitofanya mazungumzo ya amani na waasi wanaoshutumiwa kwa mauwaji ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Idriss Deby, jambo linalotia wasiwasi kwa waasi hao kuongeza jitihada za mapambano yao kutaka kuudhibiti mji mkuu wa taifa hilo,
Katika taarifa iliotolewa kwa njia ya televisheni, msemaji wa jeshi la Chad, Jenerali Azem Bermandoa Agouna amesema waasi wana mpango wa kushirikiana na makundi kadhaa ya wenye itikadi kali na mamluki wanaofanya biashara haramu ya usafirishaji watu nchini Libya.
Amesema hali hiyo inahatarisha usalama wa Chad na eneo zima la Sahel, kwa hivyo huo sio wakati wa kufanya majadiliano na wanaokiuka sheria.
Taarifa hiyo ya msemaji wa jeshi imetolewa siku moja baada ya ile ya msemaji wa kundi la waasi nchini humo lijulikanalo kama Front for Change and Concord in Chad, kusema kwamba kundi hilo liko tayari kuendesha mazungumzo na jeshi kwa ajili ya kipindi cha mpito.
''Mazungumzo sio kwa sababu tumeshindwa na vita''
Kwenye mahojiano na DW, Kingabe Uguzé Paul msemaji wa waasi amesema msisamo huo wa jeshi wa kukataa mazungumzo umewapa nafasi ya kuendelea na vita.
''Tulikubali mazungumzo sio kwa sababu tumeshindwa na vita, bali ni matakwa ya raia wetu. Licha ya uhalifu wote wanayofanyiwa na utawala wa Chad, lakini raia wetu wanataka kuweko na mazungumzo ili kuepusha umwagikaji wa damu mjini N'djamena na kote nchini.''
Toka Ijumaa baada ya mazishi ya Rais Idriss Deby, marais wa nchi tano za ukanda wa Sahel, wanaendesha juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kuweko na serikali ya mpito itakayojumuisha pande husika katika mzozo wa Chad. Marais wa Niger na Mauritania walikutana na viongozi wa kijeshi, wale wa upinzani na asasi za kiraia kwa ajili ya kuweko na kipindi cha mpito nchini Chad.
Mwito wa maandamano ya kupinga uongozi wa jeshi
Upinzani na asasi za kiraia vimeomba kuweko na serikali ya kirai kulingana na katiba ya Chad. Succès Masra ni moja ya viongozi wa upinzani nchi humo amesema wameitisha maandamano kesho kupinga utawala wa kijeshi.
''Inatakiwa kuwepo na rais ambaye sio mawanajeshi, na makamu wake anaweza kuwa mwanajeshi ambaye atahusika na masuala ya kiusalama na ulinzi. Tunatakiwa kuheshimu katiba na mkataba wa Umoja wa Afrika unaolaani mapinduzi ya kijeshi.''
Upinzani umesema kipindi cha mpito cha miezi 18 ni kirefu mno. Kwa upande wake chama tawala kimeunga mkono kuweko na kipindi cha mpito kinachoongozwa na Mahamat Deby mwanae Idriss Deby.