CENI yatathmini hali ilivyo Beni na Butembo kuandaa uchaguzi
26 Februari 2019Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi ya DRC Corneille Nangaa akamilisha ziara yake katika miji ya Beni na Butembo ambako utaandaliwa uchaguzi wa wabunge, baada ya uchaguzi kuahirishwa katika eneo hilo Desemba 30 Mwaka jana, kutokana na mapigano pamoja na homa ya Ebola.
Ziara ya Corneile Nangaa katika eneo hilo la kaskazini la mkoa wa Kivu, imewapa matumaini wakaazi, waliokuwa wamekata tamaa, kutokana na hatua ya tume huru ya uchaguzi kuwanyima haki ya kumchagua rais wampendae pamoja na wabunge.
Hatua ya kuahirisha uchaguzi katika mji na wilaya ya Beni pamoja na mji wa Butembo, Ikiwa ilifuatia mapigano ya kila mara katika mji na wilaya ya Beni pamoja na homa ya Ebola, mwenyekiti wa CENI amesema, kuwa hali imebadilika na kwamba tume yake iko tayari kuandaa uchaguzi Machi 31.
"Napatikana katika eneo hili la kaskazini kubwa la mkoa wa Kivu ya kaskazini, kukadiria hall ya kiufundi kwa ajili ya maadalizi ya uchaguzi hapa, na tumefanya hilo ili Machi 31 tuende kwenye uchaguzi kwani raia wanasubiri uchaguzi huo na ni jambo la kwanza linalotupatia matumaini. Na taarifa nzuri ni kwamba, hali iliyotupelekea kuahirisha uchaguzi imebadilika kwa kiwango kikubwa." Amesema Nangaa.
Mapigano ya kila mara katika eneo hili pamoja na homa ya Ebola, vikiwa vimeshawapelekea wakaazi wengi kuyahama makazi yao nakukimbilia mahala pengine, na ikiwa ni vigumu kwao kurudi katika maeneo walikojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika wilaya ya Beni Noella Muliwavyo alimuomba Nangaa kuwaruhusu wakimbizi kupiga kura walikokimbilia.
Hata hivyo ombi lake halikukubaliwa na mwenyekiti wa CENI, jambo lililomkasirisha bi Noaella Muliwavyo aliyesema:
"Hakujibu ipasavyo kwa maswali yetu kwani tulipendekeza kuwa wakaazi wote wa wilaya ya Beni wapigie Kura wanakopatikana kwani kuna wakimbizi wa ndani na haiwezikani mtu kurudi jumbani alikotoka kwaajili ya kupiga kura. Ingelikuwa yetu furaha kuona mwenyekiti anatuelewa na kuruhusu wakimbizi kupiga kura walikokimbilia."
Wagombea ubunge wa kitaifa na kimikoa, watapewa wiki mbili za kampeni, ili kuwakumbusha wapiga kura namba zao, pamoja na vyama vyao vya kisiasa.
Na jipya katika uchaguzi wa Machi 31 ni kwamba, ofisi ya mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi CENI itahamishwa kuja Beni, jambo litakalompelekea mwenyekiti wa tume hiyo pamoja na wasaidizi wake kufuatilia kwa karibu sana zoezi la upigaji kura.
Uchaguzi wa gavana wa mkoa wa Kivu ya kaskazini, umetangazwa kuwa utafanyika, baada ya wakaazi wa mji na wilaya ya Beni pamoja na mji wa Butembo kupiga kura, na kwa hiyo kuwapa nafasi wabunge watakaochaguliwa kuchangia katika uchaguzi wa gavana.