1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU yaibwaga SPD katika jimbo la Schleswig- Holstein

8 Mei 2017

Chama cha kansela Angela Merkel cha Chirstian Democtratic Union kimepata ushindi katika jimbo la kaskazini la Schleswig-Holstein kwenye uchaguzi wa majimbo uliofanyika jana hapa nchini Ujerumani

https://p.dw.com/p/2carO
Deutschland Daniel Günther CDU Wahlen Schleswig-Holstein
Picha: REUTERS/F. Bimmer

Chama hicho cha kihafidhina cha CDU kinachoongozwa na Kansela Merkel kiliongoza kwa asilimia 32.8 ya kura kikiwa mbele ya wapinzani wake wa chama cha Social Democratic, SPD, ambao walikuwa ndio wanalishikilia jimbo hilo pamoja na vyama vya Kijani na chama kidogo cha SSW kinachowawakilisha wapiga kura wachache wenye asili ya Kidenmark. SDP ilipata asilimia  27.2 ya kura. 

Uchaguzi huu unachukuliwa kama ndiyo firimbi ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwezi Septemba hapa nchini Ujerumani. Ushindi huo kwa chama cha CDU cha Kansela Merkel ni pigo kwa chama cha SPD kilichokuwa kikiongoza jimbo hilo la Schleswig-Holstein lenye takriban watu milioni 2.8 tangu mwaka 2012.

Mgombea wa chama cha kihafidhina cha CDU, Daniel Guenther, baada ya kutangazwa mshindi alisema sasa anaanza mazungumzo ya kuunda serikali na vyama vyengine.  Guenther alisema ni dhahiri kuwa wao wamepewa mamlaka ya kuunda serikali ya jimbo hilo. Na hivyo watawasiliana na chama cha FDP kwa ajili ya mazungumzo ya kuunda serikali kwa pamoja na kama mazungumzo hayo hayataleta tija basi wanaweza pia kuwasiliana na chama cha Kijani cha walinda mazingira. Lakini ni wazi kuwa watu wa jimbo hilo wanataka mageuzi katika serikali na ndio maana wamekichagua chama cha CDU.

Deutschland Martin Schulz Wahlen Schleswig-Holstein
Kiongozi wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: picture alliance/AP Photo/dpa/M. Schreiber

Matokeo hayo katika jimbo la kaskazini la Schleswig-Holstein ni pigo pia kwa mpinzani mkuu wa Kansela Merkel kwenye uchaguzi mkuu wa Septemba, mgombea ukansela wa SPD, Martin Schulz. Lakini licha ya ushindi huo wa chama cha kihafidhina cha CDU bado haijulikani chama cha SPD kitafanya mazungumzo na chama gani ili kujaribu kuunda serikali. Chama cha kijani kilipata asilimia 12.9 na chama cha Waliberali cha FDP kinachoshikilia nafasi kubwa ya kuunda serikali na chama cha CDU kilipata asilimia 11.5 ya kura.  Kimsingi chama cha CDU kinaweza kuunda serikali kwa wingi wa viti 42 katika bunge lenye viti 69.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, vijana wenye umri wa miaka 16 pia walipata fursa ya kushiriki katika zoezi la kupiga kura. Maswala muhimu yaliyopewa kipaumbele zaidi katika kampeni yalikuwa ya elimu, miundombinu na maendeleo ya nishati ya upepo.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef