CDU waunga mkono Mkataba wa kuunda serikali pamoja na SPD
26 Februari 2018Kizingiti kikubwa zaidi katika zahma ya kisiasa inayopiga tangu miezi mitano iliyopita katika taifa hili lenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi barani Ulaya, kitachomoza marchi nne inayokuja yatakapojulikkana matokeo ya kura waliyopiga wafuasi wa chama cha Social Democrat na kutamka kama wanaunga mkono au la makubaliano hayo. Hakuna hadi dakika hii anaeweza kuashiria matokeo ya kura hiyo yatakuwa ya aina gani.
Mkutano wa kamati kuu ya chama cha CDU mjini Berlin umeunga mkono uamuzi wa kansela Merkel wa kuwateuwa wanasiasa vijana kushriki katika serikali mpya ya muungano ,lengo likiwa pia kuleta damu mpya katika chama hicho kinachozongwa na mabishano juu ya namna ya kukabiliana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani" AfD" na kuwavutia zaidi wapiga kura.
"Tunataka kuchangia kuwa na serikali imara yenye uwezo wa kuwajibika" amesema kansela Merkel na kusisitiza wananchi wanategemea hayo kutoka kwao. Kansela Merkel amefafanua kwa kupiga kura leo hii mkataba wa kuunda serikali ya muungano, miezi mitano baada ya uchaguzi mkuu ni ushahidi timamu wa hali tete ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali humu nchini. Kansela Angela Merkel ameendelea kusema: "Tunaweza, hasha, tunabidi tuamuwe, tunataka, tukizingatia yote yanayotokea ulimwenguni, kuwa na usemi, tunataka kuwa na makampuni yanayoongoza ulimwenguni, tunataka kuwa na uchumi unaofana ulimwenguni, au tunataka kuwaachia wengine, na sisi tukibakia kutumbua macho, licha ya kutambua madhara yanayotokana na hali hiyo, naiwe upande wa nafasi za kazi, usalama wa jamii na hali ya kuwategemea wengine. Jibu la CDU ni bayana: Tunataka Ujerumani iendelee kufanikiwa miaka inayokuja."
Kansela Merkel achambua majukumu ya serikali mpya
Katika hotuba yake kansela Merkel amewahakikishia wajumbe serikali mpya inapaswa ijiepushe na mikopo ziada, iepuke kupandisha kodi, ifanye juhudi za kuuimarisha umoja wa Ulaya, kuhakikisha mtandao wa internete unaenea kila mahala nchini Ujerumani hadi ifikapo mwaka 2025, kuzidisha gharama za shughuli za utafiti, kubuni nafasi 8000 za wauguzi na kufuata msimamo mkali "bila ya huruma" linapohusika suala la usalama.
Baada ya kuunga mkono mkataba wa kuunda serikali ya muungano pamoja na SPD, wajumbe 1000 wa CDU wanaokutana tangu asubuhi mjini Berlin watamuidhinisha pia bibi Annegret Kramp-Karrenbauer kuwa katibu mkuu wa chama hicho. Akipewa jina la utani kama "Bibi Merkel m dogo, waziri mkuu huyo wa ajimbo la Saarland, mwenye umri wa miaka 55 anapewa nafasi nzuri pia ya kumrithi Angela Merkel atakapoamua kustaafu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo