CDU/CSU na FDP kuunda serikali .
28 Septemba 2009Wapiga Kura nchini Ujerumani wameamua kumpa muhula wa pili wa uongozi Kansela Angela Merkel na kibali cha kuunda serikali mpya pamoja na chama cha Free Democrats FDP kinachopendelea biashara huria na ambacho kinatarajia kupunguzwa kodi ili kuinua uchumi. Wahafidhina Christian Democrats CDU wakiongozwa na Bibi Merkel na chama ndugu cha Christian Social Union CSU cha Mkoa wa Bavaria walikua katika serikali ya mseto kwa miaka minne iliopita na Social Democrats SPD. Hivi sasa Bibi Merkel anaelekea kuondokana na vikwazo vya ushirika huo na kuunda serikali na FDP, muungano ambao amedai ni mwafaka kwa uchumi wa Ujerumani, taifa kubwa la kiuchumi barani Ulaya.
Kwa mujibu wa matokeo hadi sasa CDU na CSU kwa pamoja vimepata asili mia 33.6 ya kura, FDP 14.5 asili mia, SPD 23.1, Linke 12.1 na Grüne chjama cha walinzi wa mazingira asili mia 10. Ni dhahiri CDU/CSU na FDP wataunda serikali ya muungano.
Serikali ijayo Itapaswa kudhibiti nakisi katika bajeti yake na kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa ajira. Vyama hivyo CDU na FDP ambavyo kwa mara ya mwisho vilitawala pamoja kuanzia 1982 hadi 1998 wakati Helmut Kohl alipokua Kansela vitapaswa kuondoa tafauti wakati wa mazungumzo yao ya muundo wa serikali ya mseto,kuhusu kiwango na wakati wa kupunguzwa kodi. Changamoto nyengine kubwa kwa serikali hiyo mpya itakua ni kudhibiti nakisi katika bajeti yake na kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa ajira.
Mwandishi:M.Abdul-Rahman /rtr
Mhariri:Sekione Kitojo