CCM, UKAWA zachuana vikali
2 Oktoba 2015Kwa mara ya kwanza chama tawala, CCM, kinakabiliwa na uwezekano wa kushindwa kwenye uchaguzi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli, amejikuta na kibarua kigumu sana katika jitihada zake za kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye anaondoka madarakani baada ya kumaliza mihula yake yake miwili anayoruhusika kikatiba.
Magufuli, mwenye umri wa miaka 55, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa upinzani, Edward Lowassa, ambaye anasimama kwa niaba ya vyama vinne vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Lowassa, mwenye umri wa miaka 62, alikiacha chama chake cha zamani, CCM, na kujiunga na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kuongoza muungano huo wa vyama mwezi Julai.
"Wagombea wote wawili wanaonekana kuelezea sera zinazofanana... kama vile kupambana na ufisadi, kukabiliana na umasikini, kutatua matatizo ya ukosefu wa ajira na mizozo ya ardhi," mhadhiri wa siasa kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana, aliliambia shirika la habari la AFP.
Mchuano ni kati ya UKAWA na CCM
Kuna wagombea wengine sita kwenye nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano kando na Lowassa na Magufuli, na wengine 12 kwa nafasi ya urais wa Zanzibar kando ya rais wa sasa, Ali Mohammed Shein kutoka CCM, na makamu wake wa kwanza, Seif Sharif Hamad kutoka Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni sehemu ya UKAWA.
Hata hivyo, ni kampeni za Lowassa na Hamad, kwa upande mmoja, na Magufuli na Shein, kwa upande mwengine, ndizo zinazovutia maelfu ya wananchi kwenye mikutano yao, tabia iliyopewa jina la "mafuriko".
Wakati anajiunga na upinzani, Lowassa alishahudumu kwenye nafasi mbalimbali katika serikali ya CCM, ikiwemo ya uwaziri mkuu baina ya mwaka 2005 na 2008. Naye Magufuli amekuwa waziri kwenye wizara mbalimbali kwa takribani miongo miwili, na hadi sasa anashikilia nafasi ya uwaziri wa ujenzi kwenye serikali ya Rais Kikwete.
Kwa upande wa Zanzibar, viongozi wawili wakuu wa serikali ya umoja wa kitaifa iliyoanzishwa baada ya uchaguzi wa 2010, Rais Shein kutoka CCM na Makamu wa Kwanza wa Rais Hamad kutoka CUF walichuana pia kwenye uchaguzi huo, ambapo Shein alimshinda Hamad kwa chini ya asilimia moja ya kura.
Ingawa wagombea wote wakuu wamekuwa wakitoa wito wa kudumishwa kwa amani na umoja wa kitaifa na wakijitenga na ukabila na udini kwenye hotuba zao, wachambuzi wanasema khofu zilizopo ni za kweli.
Wachambuzi hao wanaonya kwamba mchuano huu mkali na usio wa kawaida unaweza ukaibua hali ya wasiwasi katika taifa hilo kubwa kieneo na kwa idadi ya watu Afrika Mashariki, ambalo limezowea kuitwa la amani na utulivu.
Ukosefu wa usalama visiwani Zanzibar
Sambamba na kinyang'anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi mkuu huu unashirikisha pia viti vya ubunge na udiwani kwa upande wa Tanzania Bara, na pia uchaguzi wa urais, uwakilishi, ubunge na udiwani kwa upande wa Zanzibar, eneo la Jamhuri ya Muungano lenye utawala wake wa ndani.
Tayari matukio ya mashambulizi ya hapa na pale yameripotiwa katika kisiwa kikuu cha Unguja, ambako mwandishi wa Deutsche Welle anasema watu wanaoficha nyuso zao na wanaohusishwa na makundi ya vijana wa CCM wanavamia maeneo yanayotambuliwa kuwa ya upinzani, ambako hupiga, kujeruhi na kuharibu mali za raia.
Katika kila tukio kama hilo, jeshi la polisi visiwani humo husema linaendelea na uchunguzi, huku CCM, ambacho ni chama kikuu kwenye serikali ya umoja wa kitaifa, ikikanusha kuhusika na makundi hayo.
Hata hivyo, ushahidi uliotolewa hadharani hivi karibuni na CUF, ambacho ni chama kidogo kwenye serikali hiyo ya umoja wa kitaifa, ulitaja kuwepo kwa makambi ya vijana hao katika maeneo ya Tunguu, Dunga, Welezo na Amani, ambayo kwa pamoja yanahifadhi vijana wapatao 1,500, huku kikidai kuwa kina taarifa za makambi kama hayo kufunguliwa kwenyemaeneo ya Kilombero, Pangatupu, Bumbwini na Makunduchi.
Mabadiliko hayekwepeki
"Ingawa CCM ilionekana kuwa na fursa kubwa za kushinda uchaguzi, lakini kuna dalili kubwa kwamba uwezo wake wa kusalia madarakani unaendelea kutoweka," mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani, Johnnie Carson, aliandika kwenye jarida la mtandaoni la African Arguments.
"Matokeo ya uchaguzi yakiwa yanayokaribiana sana au kukiwa na mashaka ya wizi wa kura kunaongeza uwezekano wa ghasia za baada ya uchaguzi katika taifa ambalo limekuwa likichukuliwa linaongoza kwa demokrasia na amani barani Afrika," anasema Carson.
Hata hivyo, wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa mabadiliko hayawezi kuepukika nchini Tanzania. Rais Kikwete anaondoka madarakani kwa kuheshimu matakwa ya kikatiba, kinyume na marais wenzake kwenye mataifa jirani.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alikataa wito wa ndani na nje ya nchi yake kuondoka madarakani na akashinda uchaguzi wa muhula wa tatu mwezi Julai.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda anaamini kuwa kwa "Afrika suala la ukomo wa uongozi madarakani si jambo muhimu" na anatazamiwa kuwania tena kwenye uchaguzi wa mwakani.
Rais Paul Kagame wa Rwanda na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaaminika kutaka kuwania tena nyadhifa zao.
Kwa hivyo, hata kitendo pekee cha Kikwete kuondoka madarakani, bila ya kujali nani anaingia baada ya yeye, kinatosha kuashiria kuwa mabadiliko hayaepukiki.
Umasikini bado tatizo kubwa
Licha ya ukuwaji mzuri wa kiuchumi, kumekuwa na jitihada ndogo kabisa za kuupeleka ukuwaji huo kwa Watanzania walio wengi na bado nchi hiyo imeendelea kuwa masikini sana kwa viwango vya kieneo na kimataifa, inasema Benki ya Dunia.
Kilimo ndio sekta kuu ikiwa inazalisha robo ya pato jumla la nchi na kuajiri robo tatu ya wananchi, lakini ndio sekta iliyopuuzwa kabisa. Katika makala yake ya hivi karibuni, taasisi ya kimataifa ya Open Society ilionya kuwa "ile hali ya 'ukawaida' nchini Tanzania iko hatarini."
"Huku theluthi mbili ya raia milioni 50 wakiishi kwenye umasikini, ni wachache tu wanaofaidika na ukuwaji mkubwa wa uchumi ambao umefikia kiwango cha asilimia saba kwa muongo mmoja uliopita."
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman