Catalonia na Suala la Wahamiaji nchini Uerumani , Magazetini
13 Februari 2019Tunaanza na kesi ya aina pekee kuwahi kushuhudiwa tangu enzi za muimla Franco zilipomalizika nchini Uhispania. Korti kuu ya Uhispania mjini Madrid imeanza kusikiliza kesi dhidi ya wanasiasa na wanaharakati 12 waliotangaza kujitenga jimbo la Uhispania la Catalonia Octoba mwaka 2017. Gazeti la "Reitlinger General-Anzeiger" linaandika: "Mashitaka yanazungumzia kuhusu uasi, yanakwenda umbali wa kuzungumzia uhaini na matumizi mabaya ya mali ya umma. Kiini litakuwa suala kama madai ya uasi ni ya kimsingi. Eti uasi unaweza kufungamanishwa na matumizi ya nguvu na kama kuna uwezekano wa kuasi kwa amani?
Kishindo chengine cha kusitishwa shughuli za serikali chaepukwa chupu chupu
Bunge la Marekani Congress limefanikiwa kuepusha kishindo chengine cha kufungwa ofisi za serikali kufuatia mvutano kati ya wademocrats na rais Donald Trump kuhusu ujenzi wa ukuta kuitenganisha Marekani na Mexico. Gazeti la "Südwest Presse" linaandika:"Pekee ule ukweli kwamba wa-Republicans na wa-Democrats wamefikia maridhiano kuhusu bajeti ili kuepusha kishindo chengine cha kusitishwa shughuli za idara za serikali ni majabu. Maridhiano hayo hayakuchochewa lakini na utayarifu wa kutotanguliza mbele misimamo ya vyama vya kisiasa. Pande hizo mbili zimetambuwa tu hakuna faida yoyote watakayoipata, kinyume kabisa, pande zote mbili zitakula hasara."
Wahamiaji wana faida kwa Ujerumani
Suala la wahamiaji linaendelea kuzusha mfarakano katika jamii nchini Ujerumani. Hata hivyo uchunguzi uliochapishwa umebainisha Ujerumani inahitaji wahamiaji. Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" limemulika uchunguzi huo na kuandika:"Tunahitaji wahamiaji 260.000 kwa mwaka, zaidi ya nusu ni wa kutoka nchi ambazo si wanachama wa Umoja wa Ulaya. Hayo yametajwa na wataalamu katika ripoti yao iliyochapishwa hivi punde. Hilo lakini wananchi ambao baadhi yao bado wana kihoro kufuatia wimbi la wahamiaji la mwaka 2015, wanabidi waelezwe. Haki ya ukimbizi kwa mfano haihusiani hata kidogo na wahamiaji wenye ujuzi wa kazi, jamii hizo mbili mara nyingi hutumbukizwa ndani ya chungu kimoja ingawa kisheria makundi hayo mawili ni tofauti kabisa. Na zaidi ya hayo historia imetufunza Ujerumani kwa miongo kadhaa imekuwa ikifaidika kutokana na wahamiaji."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga