1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Carla Del Ponte avunjika moyo kutokana na hali ya Syria

Oumilkheir Hamidou
7 Agosti 2017

Mwendesha mashitaka mkuu wa zamani wa korti ya kimataifa ya uhalifu wa vita, bibi Carla Ponte ajitoa katika tume huru ya Umoja wa Mataifa inayochunguza vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria.

https://p.dw.com/p/2hoRi
Carla del Ponte gibt ihren Posten in der Uno-Untersuchungskommission für Syrien ab
Picha: picture alliance/AP Photo/M. Trezzini

Katika maelezo yaliyochapishwa jana na jarida la Uswisi, Blick, Del Ponte ameelezea jinsi alivyovunjwa moyo na tume hiyo na kuikosowa tangu serikali ya rais Bashar al Assad, upande wa upinzani pamoja pia na jumuia ya kimataifa.

"Hatujafanikiwa hata kidogo" ameliambia jarida la Blick pembezoni mwa maonyesho ya filamu ya  Locarno jana."Kwa miaka mitano tumekuwa tukikumbana na vizingiti tu."Amesema.

Carla del Ponte aliyejipatia umaarufu alipokuwa mwendesha mashitaka mkuu wa korti ya kimataifa ya iliyochunguza uhalifu wa vita nchini Rwanda na Yugoslavia, amelikaripia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kushindwa kuunda korti kama hiyo kushughulikia vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea tangu miaka sita na nusu iliyopita nchini Syria. Urusi ambayo ni mwanachama wa kudumu na mwenye hakai ya kutumia kura ya turufu, ni mshirika mkubwa wa serikali ya rais Assad.

Maafa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria
Maafa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/A. Alhalabi

Jumuia ya kimataifa yakosolewa na Del Ponte

"Nnaachilia mbali, mataifa ya baraza la Usalama hayataki haki" amesema Del Ponte na kuongeza anapanga kushiriki katika mkutano wa mwisho mwezi unaokuja wa Septemba."Siwezi kuendelea kuwa mwanachama wa tume ambayo haifanyi chochote."

Akichaguliwa septemba mwaka 2012, Carla Del Ponte amenukuliwa na jarida la Blick akisema anahisi kilikuwa "kisingizio tu" kumkabidhi jukumu katika tume hiyo."Nimeshaandika risala ya kujizulu na nitaituma siku zinazokuja" amesema.

Katika uchambuzi wake kwa jarida la Blick, Carla Del Ponte ameitaja Syria kuwa ni nchi isiyokuwa na "mustakbali."

"Uhalifu nilioushudia Syria, sijawahi kuuona kokote kwengine, si Rwanda na wala si katika  Yugoslavia ya zamani" amesema na kuongeza," tulifikiri jumuia ya kimataifa imejifunza kutokana na yaliyotokea Rwanda. Lakini la, haikujifunza chochote."

Watoto waliolazimika kuyapa kisogo maskani yao kwasababu ya vita
Watoto waliolazimika kuyapa kisogo maskani yao kwasababu ya vitaPicha: Reuters/B.Khabieh

 Tume huru ya Umoja wa mataifa itaendelea kuwaandama na kuwafikisha mahakamani wahalifu

Baada ya kupita miaka sita ya vita nchini Syria, Carla Del Ponte anasema "kila mtu ni mbaya nchini Syria, tangu serikali mpaka upande wa upinzani."

Tume huru ya kimataifa inayochunguza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria imesema katika taarifa yake imekuwa ikijua tangu kati  kati ya mwezi wa juni kama Del Ponte anapanga kujiuzulu na kusisitiza wataendelea na jukumu lao la kuwafikisha mahakamani wahalifu wote wa vita nchini Syria. Kujiuzulu Del Ponte kunaifanya tume hiyo ipungukiwe na wanachama wawili baada ya kujitoa mwaka jana mwanaharakati wa haki za binaadam Vitit Muntarbohrm na kujiunga na tume huru ya Umoja wa Mataifa inayoshugulikia matumizi ya nguvu na ubaguzi ulioshawishiwa kijinsia.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri: Mohammed Khelef