CANNES : Merkel ataka Waafrika kutatuwa migogoro yao
16 Februari 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amezitaka nchi jirani na Zimbabwe kutumia ushawishi wao kusaidia kumaliza shida za wananchi wa nchi hiyo zilizosababishwa na sera za Rais Robert Mugabe.
Akizungumza katika Mkutano wa Viongozi kati ya Ufaransa na Afrika katika mji wa mapumziko ya kitalii wa Cannes nchini Ufaransa Merkel amesema wamekuwa wakiangalia hali ya Zimbabwe kwa wasi wasi mkubwa ambako kumekuwepo na kutishiwa kwa wapinzani wa kisiasa,dhiki, vitisho dhidi ya wakulima na kuteketezwa kwa makaazi ya vitongojini wanakoishi maskini.
Merkel amewaambia washiriki wa mkutano huo kwamba hakuna haki kabisa ya kuhalalisha mambo hayo.
Ikibadili msimamo wa Mkutano wa Viongozi wa Ufaransa na Afrika uliopita wa mwaka 2003 Ufaransa safari hii imeamuwa kutomwalika Rais Mugabe katika mkutano huo wa Cannes.
Rais Jaques Chirac wa Ufaransa pia ameuhutubia mkutano huo na kutowa wito kwa serikali ya Sudan na waasi kukubali uwekaji wa kikosi cha kulinda amani cha kimataifa katika jimbo lililoathiriwa na vita la Dafur.
Takriban viongozi 30 wa Afrika na Kansela wa Ujerumani ambaye nchi yake hivi sasa inashikilia Urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya wameungana na Rais Chirac katika mkutano huo.