CANBERRA:Msitishwe na Mugabe
1 Desemba 2003Australia leo imeitaka Jumuiya ya Kimataifa isikubali kutisha na Rais Robert Mugabe aliyetishia kujitowa kwenye Jumuiya ya Madola iwapo uwanachama wake utatishia haki ya kujitawala kwa nchi hiyo. Waziri wa mambo ya nje wa Australia Alexander Downer amesema hali nchini Zimbabwe inazidi kuwa mbaya na Mugabe hakuchukuwa hatua yoyote ile ya kuishajiisha jumuiya hiyo ya makoloni mengi ya zamani ya Uingereza kuiondolea kikwazo cha kusitishwa uwanachama wake. Zimbabwe ilisitishwa uwanachama wa Jumuiya ya Madola yenye nchi wanachama 54 hapo mwaka jana baada ya Mugabe kushutumiwa kwa kuhujumu uchaguzi wa Rais wa kuwania kuchaguliwa tena.Kiongozi huyo wa Zimbabwe hakualikwa katika Mkutano wa Viongozi wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliopangwa kufanyika mjini Abuja Nigeria kuanzia Desemba tano hadi nane. Suala la Zimbabwe lilihodhi maadalizi ya mkutano huo wa viongozi wa Jumuiya ya Madola na kutishia kuigawa jumuiya hiyo kwa misingi ya kikabila.