Canberra. Waziri Howard ahidi kutuma vikosi zaidi Afghanistan.
13 Julai 2005Waziri mkuu wa Australia Bwana John Howard amesema kuwa nchi yake itatuma vikosi maalum vya wanajeshi 150 pamoja na vikosi vya usaidizi kwenda Afghanistan.
Bwana Howard amewaambia waandishi wa habari mjini Canberra leo kuwa vikosi hivyo vitasaidia majeshi ya Marekani kuwasaka wapiganaji wanaojitokeza tena wa Taliban na al Qaeda.
Amesema kuwa Australia pia itaangalia uwezekano wa kutuma watu 200 zaidi nchini Afghnistan mapema mwaka ujao kusaidia katika ujenzi mpya na kama sehemu ya juhudi zaidi za nchi yake za kusaidia vita dhidi ya ugaidi.
Hakuna mabadiliko yanayopangwa katika vikosi vya sasa vya jeshi la nchi hiyo vilivyoko Iraq, ambako majeshi ya Australia yanawanajeshi wanaofikia 1,300.