1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Canada yatishia kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Afghanistan

29 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CyzV

Waziri mkuu wa Canada, Stephen Harper, ametishia kuwaondoa wanajeshi 2,500 wa nchi hiyo kutoka Afghanistan mapema mwaka ujao ikiwa washirika wa jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi NATO, hawatapeleka angalu wanajeshi 1,000 zaidi kusini mwa Afghanistan kukabiliana na wanamgambo wa Taliban.

Harper amesema kushindwa kwa jumuiya ya NATO kupeleka wanajeshi wa kutosha nchini Afghanistan kunahatarisha ufanisi wa harakati za kijeshi nchini humo.

Hatua ya washirika wa Ulaya kukataa kupeleka majeshi katika eneo hatari la kusini mwa Afghanistan kumesabisha tofauti kubwa kati yao na Uingereza, Canada, Uholanzi, Marekani na nchi nyingine, ambazo zimepata hasara kubwa kutokana na machafuko ya wanamgambo wa Taliban.

Wakati huo huo, Marekani imetaka mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghansitan ateuliwe haraka baada ya mwanasiasa wa Uingereza, Paddy Ashdown, kuondoka nchini humo kwa kile anachokiita hatua ya serikali ya Kabul kutomuunga mkono kikamilifu.