1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameroon na Ghana kuumana nusu fainali

Sekione Kitojo
2 Februari 2017

Nusu fainali ya pili katika  kombe la mataifa ya Afrika nchini Gabon, Afcon inafanyika leo, mabingwa mara nne Cameroon wakipambana na mabingwa mara nne pia Ghana katika mpambano unaotabiriwa kuwa wa vuta nikuvute.

https://p.dw.com/p/2Ws3G
Kamerun Fußball Nationalmannschaft
Kikosi cha Simba wa Nyika Cameroon mwaka 2015Picha: P.-P. Marcou/AFP/Getty Images

Ghana   ilionekana  kujiweka  haraka  kuwa  moja  kati  ya  vigogo vya  soka  barani  Afrika   tangu  kuanzishwa  mashindano  hayo, baada   ya  Misri  kutawala  soka  la  Afrika   miaka  miwili  ya mwanzo tangu  mashindano  hayo  yaliapoanzishwa  mjini  Addis Ababa  mwaka  1957.

Ghana  ilijiunga  na  mashindano  hayo  na  kulinyakua  kombe  hilo kutoka  kwa  Misri  mwaka  1963 na  kulinyakua  tena  mwaka  1965, 1978  na 1982. Tangu  wakati  huo Ghana  ilipotea  kutoka  katika kundi  la  vigogo vya  soka  barani  Afrika  na  imefanikiwa  tu kuingia  katika   fainali  mara  mbili  katika  miaka  ya  2000, lakini haijaonja  tamu  ya  kurejea  nyumbani  na  taji  hilo la  bara  la Afrika.

Ghana Fußball Nationalmannschaft
Kikosi cha timu ya taifa ya GhanaPicha: F. Leong/AFP/Getty Images

Cameroon  nayo  ikijivunia  rekodi  ya  kulinyakua  kombe  hilo  mara nne  pia  inawania  mara  hii  kulipeleka  taji  hilo  mjini  Yaoude  kwa mara  ya  tano. Cameroon  ililinyakua  kombe  hilo mara  ya  kwanza mwaka  1984  na  kisha  mwaka  1988, 2000  na  2002.

Cameroon  ilitokea  kutoka  kundi  A  katika  mashindano  ya  mwaka huu ikifungwa  katika  mchezo  wa  kwanza  na  Jamhuri  ya Kidemokrasi  ya  Congo  kwa  bao 1-0  na  kisha ikaishinda  Guinea ya  Ikweta  kwa  mabao 2-1, na  kutoka  sare  na wenyeji  wa mashindano  hayo  Gabon  bila  kufungana ikijitokeza  kuingia  duru ya  robo  fainali  ikiwa  namba  mbili  kutoka  kundi  hilo.  Cameroon ilionesha  makali  yake  pale  ilipofanikiwa  kuitoa  kwa  mikwaju  ya penalti Senegal  katika  mchezo  mkali  na  wa  kuvutia wa  robo fainali  baada  ya  timu  hizo  kucheza  kwa  dakika  120  bila kufungana.

Safari  ya  Cameroon

Njia  ya  Cameroon  kuelekea  nusu  fainali  haionekani  kuwa  rahisi hivyo  kwani  ilipata  ushindi  mara  moja  tu  wa  wazi  dhidi  ya  timu ndogo  ya  Guinea  ya  Ikweta, lakini  pia  kuishinda  Senegal ambayo  ilipigiwa  upatu katika  duru  ya  makundi  kwamba  huenda ndio  itatawazwa  mabingwa   katika  fainali  hizi  si  jambo  la kubezwa. 

FIFA Fußball WM 2014 USA Ghana
Nahodha wa Ghana Andre AyewPicha: picture-alliance/dpa

Inadhihirika  wazi  kwamba  Cameroon  mara  hii  ni  imara  zaidi katika  ulinzi  kuliko  ushambuliaji , lakini  timu  yoyote  inayoweza kuwasimamisha  washambuliaji  hatari  wa  Senegal , kina  Sadio Mane , na  Biram Diouf Mame inahitaji  ukuta  imara  ambao utatumika  hata  leo  kuwazuwia  washambuliaji  hatari  wa  Ghana  , kina Andre Ayew  na  mdogo  wake.

Gabun Afrika Cup 2017 Senegal vs. Kamerun
Mpambano kati ya Cameroon na Senegal katika mashindano ya Afcon 2017Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Ghana ambayo  inaonekana  kimahesabu  kuwa  bora  zaidi  ya Cameroon  jioni  ya  leo  itabidi  kufanya  kazi  ya  ziada  kuuvunja ukuta  wa  Cameroon.

Ghana  iliyokuwa  katika  kundi  D , ilianza  kwa  ushindi  wa  bao 1-0 dhidi  ya  wawakilishi  kutoka  Afrika  mashariki   Uganda, ikaifunga Mali  pia  kwa  bao 1-0  na kufungwa  bao 1-0  na  Mafarao  wa Misri  lakini  ikajihakikishia  nafasi  ya  kucheza  robo  fainali  ikiwa nayo  katika  nafasi  ya  pili  nyuma  ya  Misri.

Africa Cup of Nations Training Team Ägypten
Kikosi cha timu ya taifa ya Misri katika mashindano ya Afcon 2017Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Lolote  litakalotokea  hii  leo(02.02.2017)  kati ya  Cameroon  na  Ghana , Mafarao  wa  Misri  watakuwa  wanakodoa  macho  kuona  ni  mbinu gani  watazitumia  katika  fainali  dhidi  ya  yeyote  kati  ya  timu  hizo hapo  tarehe 5 Jumapili.

Mwandishi: Sekione  Kitojo /

Mhariri: Yusuf Saumu