Cameron kuongoza seraikali mpya Uingereza
12 Mei 2010Mwenyekiti wa chama hicho cha kihafidhina David Cameron ameteuliwa waziri mkuu baada ya kujiuzulu kwa kiongozi wa chama cha Labour,Gordon Brown.Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 43,amesema,lengo lake ni kuunda serikali ya muungano uliokamilika,kati ya Conservatives na Liberal Democrats,kinachoongozwa na Nick Clegg.
Chama cha Consevatives, kilishinda kura na viti vingi, kuliko vyama vingine, katika uchaguzi mkuu uliofanywa Alkhamisi iliyopita,lakini kilishindwa kupata wingi wa kuweza kuunda serikali peke yake. Vyama vya Conservative na Labour, vilikuwa na majadiliano ya kuunda serikali pamoja na Liberal Democrats.
Ripoti zinasema, George Osbourne atakuwa waziri mpya wa fedha na kiongozi wa zamani wa chama cha Conservative, William Hague,ataongoza wizara ya mambo ya nje. Nick Clegg atakuwa Naibu Waziri Mkuu na wanachama wenzake wanne watakuwemo katika baraza la mawaziri.
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza,David Cameron, amepongezwa na viongozi wa kimataifa, baada ya kiongozi huyo wa chama cha kihafidhina kupokea madaraka kutoka kwa Gordon Brown wa chama cha Labour.
Rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwa amemuambia Cameron ataendelea na uhusiano maalum ulioko kati ya nchi zao na amemualika kiongozi huyo mpya wa Uingereza, kwenda Washington wakati wa majira ya joto. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel vile vile amempongeza Cameron na amemualika kwenda Berlin upesi awezavyo. Taarifa kutoka ofisi ya Cameron imesema, viongozi hao kwa ufupi walijadili hali ya uchumi duniani na ajenda ya pamoja ya nchi za Ulaya.
Mwandishi: P.Martin/RTRE/DPA