Mkutano wa Cameron na Merkel
29 Mei 2015Merke´l amekariwa akisema "Nitaingia kwenye mazungumzo haya kwa nia ya tija.Nataka kupata ufumbuzi na ninapofikiria jinsi tulivyoanza mazungumzo ya bajeti kwa ajili mtizamo wa kifedha wa kipindi cha kati na jinsi tulivyoweza kupata ufumbuzi huo ni mfano mzuri wa vipi tunaweza kupatanisha misimamo ambayo inaonekana haisuluhiki."
Kansela Angela Merkel ametowa kauli hiyo Ijumaa (29.05.2015) mjini Berlin pembezoni mwa David Cameron wakati waziri mkuu huyo wa Uingereza akikamilisha ziara yake ya mataifa manne ya Ulaya kushinikiza kuridhiwa kwa mpango wake wa masharti ya Uingereza kuendelea kubakia kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Merkel amesema kwamba mazungumzo yao yalikuwa na tija na ya kirafiki na kudokeza kwamba yumkini ikawa hata ni kwa maslahi ya Ujerumani kuona baadhi ya mageuzi yanafanyika katika Umoja wa Ulaya na kuongeza kwamba penye nia pana njia.
Amesema Ujerumani ina matumaini makubwa kwamba Uingereza itaendelea kubakia kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Cameron ana matumaini
Serikali mpya ya chama cha Conservative ya Cameron iliochaguliwa hivi karibuni imeahidi kuitisha kura ya maoni kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 kuhusu iwapo Uingereza iiendelee kubakia Umoja wa Ulaya au ijitowe.
Cameron ameonekana kuwa na matumaini baada ya mazungumzo yake na Merkel kwa kusema kwamba viongozi hao wawili walipata nafasi ya kulizungumzia suala hilo huko nyuma lakini mkutano huu ni fursa kuanza kulishugulikia suala hilo nukta kwa nukta.
Cameron akitahadharisha iwapo nchi hiyo haitoridhiwa madai yake ya mageuzi. amesema "Daima nimekuwa nikisema kwamba iwapo sitofanikiwa kupata chochote kile kati ya haya hapo tena chochote kile kinaweza kutokea na ninamaanisha kile ninachosema.Lakini nataraji na kuamini Ulaya itakuwa tayari kuafikiana wakati mojawapo ya nchi kubwa, mchangiaji mkubwa na mwenye sauti kubwa Ulaya anapokuwa na matatizo na masuala .....kwamba mambo hayo yanashughulikiwa ipasavyo."
Poland yaonyesha upinzani
Cameron amesema anataka Uingereza iendelee kubakia katika Umoja wa Ulaya iwapo itafanikiwa kuzungumzia upya uhusiano wake na umoja huo na kukubaliwa kudhibiti mafao ya kijamii kwa wahamiaji wanaoingia nchini mwake kutoka nchi za Umoja wa Ulaya.
Hata hivyo baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Poland Ewa Kopacz mapema Ijumaa mjini Warsaw waziri mkuu huyo wa Poland ameelezea upinzani wake mkali kwa ufumbuzi ambao utakuja kupelekea kubaguliwa kwa Wapoland au raia wengine wa nchi za Umoja wa Ulaya wanaofanya kazi kwa kuzingatia sheria nchini Uingereza.
Mamia kwa maelfu ya raia wa Poland wameloweya nchini Uingereza tokea Poland ijiunge na Umoja wa Ulaya hapo mwaka 2004.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP
Mhariri:Yusuf Saumu