CAIRO-Upande wa upinzani Lebanon wataka hatma ya Rais wa nchi hiyo iamuliwe baada ya uchaguzi wa Bunge wa Mei.
21 Machi 2005Kiongozi wa upinzani anayeheshimika nchini Lebanon,Bwana Walid Jumblatt amesema hatma ya rais wa nchi hiyo anayelindwa na Syria ni lazima iamuliwe baada ya uchaguzi wa wabunge utakaofanyika mwezi wa Mei mwaka huu.
Bwana Jumblatt pamoja na viongozi wengine wa upinzani nchini Lebanon,walimtaka Rais Emile Lahaoud kujiuzulu mara baada ya kutokea mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo,Bwana Rafik al-Hariri katika shambulio la bomu wanaloamini limetekelezwa na Syria.Hata hivyo serikali ya Syria imekanusha kuhusika na mauaji ya Bwana Hariri.
Maofisa wa Lebanon kwa upande wao wamesema kuwa Rais Lahoud kwa sasa hafikirii kujiuzulu.Juzi siku ya Jumamosi rais Lahoud alitaka kuitishwe mazungumzo ya pamoja yatakayoshirikisha upande wa serikali na upinzani,wito ambao upinzani nchini humo umeupuuza.