1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cairo. Makundi ya wapiganaji wa Kipalestina yaahidi kuacha umwagaji damu dhidi ya Israel na badala yake yanataka kupatiwa kazi.

13 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFNg

Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Silvan Shalom, ameitaka Misr kusaidia katika kuhakikisha kuwa sauti za Wapalestina wenye msimamo wa wastani zinasikika zaidi kuliko za wale wenye msimamo mkali katika Ukanda wa Gaza baada ya kuondoka kwa majeshi ya Israel.

Akizungumza mjini Cairo, pia amesema kuwa makubaliano yatafikiwa hivi karibuni kwa Misr kuipatia Israel gesi. Israel inahofia kuwa makundi ya Waislamu wenye imani kali kama Islamic Jihad na Hamas yanaweza kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na kuondoka kwa majeshi ya Israel kutoka Gaza baadaye mwaka huu.

Shalom pia ametoa wito kwa Misr kufanya juhudi zaidi kuzuwia silaha kupitishwa katika mpaka wake na kuingia Gaza.

Wakati huo huo wapiganaji zaidi ya 200 wa Kipalestina wameahidi kutofanya vitendo vya umwagaji damu dhidi ya Israel na badala yake wapatiwe kazi. Mamlaka ya utawala wa Palestina imesema kuwa inatafuta uwezekano wa kupata uhakika kwa maandishi kutoka kwa zaidi ya wapiganaji 1000 wa Kipalestina.