1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BVB yaangusha ponti, mapambano yaendelea kwingineko

21 Machi 2022

Huku kukiwa na mechi saba za Bundesliga zilizosalia msimu huu, Bayer Leverkusen na RB Leipzig zimeimarisha nafasi zao za kumaliza katika nne bora. Mkiani, Stuttgart na Hertha Berlin zinaonyesha dalili za kufufuka

https://p.dw.com/p/48nIZ
1. FC Köln - Borussia Dortmund
Picha: Dennis Ewert/RHR-FOTO/IMAGO

Kama kulikuwa na matumaini yoyote madogo ya kuwepo kinyang'anyiro kikali cha Bundesliga msimu huu, hakika yameisha sasa. Hii ni baada ya Borussia Dortmund kubanwa kwa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Cologne Jumapili jioni. Ina maana kuwa Bayern Munich sasa ina pengo la pointi sita kileleni huku kukiwa kumesalia mechi saba tu kwa msimu kukamilika. Bayern waliwalima Union Berlin mabao manne kwa sifuri katika mechi ambayo walidhihirisha utajiri wao kikosini.

Sasa ina maana Dortmund wana pointi tisa juu ya Leverkusen na 12 juu ya RB Leipzig katika nafasi ya nne ambayo mapambano ya nafasi za kucheza Champions League yanaendelea kupamba moto.

Fußball Bundesliga I VfB Stuttgart - FC Augsburg
Stuttgart wamejiondoa katika eneo la hatariPicha: Harry Langer/DeFodi Images/IMAGO

Baada ya wiki mbaya ambayo ilianza kwa kuchapwa na Cologne na kuondolewa katika Europa League mikononi mwa Atalanta, Bayer Leverkusen walirejea kwenye njia za ushindi kwa kuwafunga Wolfsburg 2 – 0 jana Jumapili na kuishikilia kwa nguvu nafasi ya tatu kwenye ligi na pointi 48.

Mapema jana, mahasimu wa nafasi nne za juu RB Leipzig walikabwa kwa sare tasa na Eintracht Frankfurt. Hata hivyo pointi hiyo ilitosha kuwaweka RB katika nafasi ya nne, baada ya Freburg kukamatwa pia kwa sare tasa na washika mkia Fürth.

Katika upande wa mkia, kuna mapambano ya pande nne ya kubaki katika Bundesliga huku Arminia Bielefeld, Hertha Berlin, Augsburg na Stuttgart zote zikiwa zimetenganishwa na pointi moja pekee. Stuttgart wanaonekana kuwa katika hali nzuri baada ya ushindi wao wa 3 – 2 dhidi ya Augbsurg, wakati Hertha waliwachabanga Hoffenheim 3-0 katika mechi ya kwanza chini ya kocha mpya Felix Magath, ambaye hakuwa uwanjani kutokana na maambukizi ya corona. Bundesliga imeingia mapumziko ya wiki mbili kupisha michuano ya kimataifa.

afp, ap, reuters, dpa