1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush katika Bunge la Israel-Knesset

Othman, Miraji16 Mei 2008

Miaka 60 tangu kuundwa dola ya Israel, mambo mengi yamegeuka kuwa kweli, mambo ambayo mwanzoni yalionekana kuwa yasingweza kufanyika.

https://p.dw.com/p/E14U
Rais George Bush wa Marekani akilihutubia Bunge la Israel-KnessetPicha: AP


Ndio maana haijawa vigumu kwa Rais George Bush wa Marekani, katika hotuba yake ya jana mbele ya bunge la Israel-Knesset- kuzungumzia zaidi juu ya wazo la mustakbali utakavokuwa kwa dola hiyo ya kiyahudi kuliko kuizungumzia hali halisi ya kisiasa ilivyo hivi sasa, angalau juu ya suala muhimu, kama kutakuweko amani baina ya Israel na Wapalastina. Umesahauliwa sasa ule mpango uliotangazwa mwaka jana unaotaka amani hiyo ipatikane mwishoni mwa mwaka huu. Badala yake George Bush alichora picha juu ya vipi miaka 60 mingine itakavokuwa kwa Israel. Amesema Israel itakuwa na amani, Wapalastina watakuwa na dola yao ya kidemokrasia na pia nchi nyingine katika eneo hilo, zikiwemo Syria na Iran, zitakuwa nchi huru za kidemokrasia.

Katika yote yanayosemwa mtu hatobisha, ila moja: Jee miaka 60 iliopita kwa Israel itakuwa kama miaka 60 ijayo? George Bush katika miaka iliopita alikuwa mtu mwenye matumaini makubwa zaidi katika kulijibu suali hilo pale alipompinduwa kutoka madarakani Saadam Hussein wa Iraq , na kutoka hapo akatangaza ile nadharia yake. Nadharaia hiyo ni kwamba kuagushwa utawala wa Saadam Hussein kutapelekea nchi nyingine katika Mashariki ya Kati nazo kuonja utamu wa demokrasia. Lakini kutoka wakati huo, mtu sasa anatambua kwamba rais huyo wa Marekani alikosea.


Mara hii, lakini, George Bush hapangi kuanzisha vita vipya. Na licha ya hayo, wakati mdogo uliobakia kwa yeye kuweko madarakani haumwezeshi kufanya hivyo. Pia wakati huo aliobakia nao haumwezeshi kuifikia amani, hata kama anaitaka. Wakati mwingi ulipotezwa katika miaka iliopita, na hadi leo George Bush hayuko tayari kusema wazi wazi na kinaganaga nini anachotarajia pande mbili- yaani Israel na Wapalastina- wafanye kwa ajili ya amani. Badala yake anazungumzia juu ya ushirika usiotikisika baina ya Israel na Marekani, anampongeza waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Ariel Sharon, kama mpiganiaji wa amani na anawaunga mkono wale wanaokataa katukatu kuwa na mawasiliano na Chama cha Kipalastina cha Hamas. Yeye anasema mtu hawezi kuzungumza na muuwaji.


Bila ya shaka, George Bush pia ana haki pale anaposhikilia kwamba haifai kuilazimisha nchi ifanye mashauriano na mtu yeyote ambaye anataka nchi hiyo kuiangamiza. Lakini uwapi mbadala kwake? Vipi juu ya kuwaunga mkono na kuwasaidia Wapalastina wanaoonesha wako tayari na wanataka amani na walio tayari kuregeza kamba? Hamna neno ambalo rais huyo alilitaja mbele ya Knesset. Katika bunge hilo, waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, alikuwa na ujasiri zaidi, licha ya malalamiko yaliotolewa na wabunge wa mrengo wa kulia, kutangaza kwamba Israel na bunge la nchi hiyo litaukubali mpango wa kuwa na dola mbili, yaani dola ya Kipalastina ikiishi ubavu kwa ubavu na dola ya Israel.


Na kwa upande wa Bush. Aliyakariri yale yale maneno yake ya zamani. Nayo ni kwamba Marekani itaendelea kuiunga mkono kikamilifu dola ya Israel, na hasa dhidi ya kile kinachoitwa vitisho vya mashambulio ya kinyukliya kutokea Iran.


Huko Saudi Arabia na Misri ambako leo anakwenda, George Bush ataeleweka zaidi sasa kuliko ilivokuwa mwezi wa Januari alipokuweko huko kuhusu mashambulio yake dhidi ya Iran. Hii inatokana na hali ya mambo ilivyo Lebanon. Lakini watawala wa nchi hizo mbili za Kiarabu pia hawaridhiki na Bush, juu ya mtindo wake wa kutia na kutoa kuhusu kuuendeleza mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati. Huko Riyadh na Cairo, na hasa huko Ramallah, Gaza na Jerusalem mtu alitarajia zaidi kutoka ziara hii ya Bush kuliko tu yeye kuzungumzia juu ya wazo la mustakbali ulio wa kiza .