Bush asema lazima mgogoro wa fedha utatuliwe haraka.
25 Septemba 2008WASHINGTON.
Mjumbe wa chama cha Republican John McCain anaegombea urais wa Marekani amesema anaahirisha kampeni ya uchaguzi na kurejea Washington ili kushughulikia mgogoro ulioyakumba mabenki na mashirika makubwa ya fedha nchini Marekani. Na kwa ajili hiyo McCain ametoa mwito wa kuahirisha malumbano na mpinzani wake Barack Obama anaekiwakilisha chama cha Demokratik katika kugombea urais.
McCain amesema huu ni wakati wa pande zote kusimama pamoja katika juhudi za kuutatua mgogoro wa fedha unaoikabili Marekani.
Lakini mpinzani wake wa chama cha Demokratik seneta Barack Obama anataka malumbano hayo yafanyike kama ilivyopangwa kwenye chuo kikuu cha Mississippi.
Wakati huo huo rais G. Bush amewaalika wajumbe hao wawili ,kuenda Ikulu ili kujadili mpango wa rais huyo wa kutenga dola Bilion 700 ili kurejesha utengemavu kwenye masoko ya fedha.Rais Bush amesema Marekani inakabiliwa na mgogoro mkubwa mkubwa sana. Akizungumza kwa njia ya televisheni rais huyo amesema kuwa shughuli za masoko haziendi vizuri na kwamba imani miongoni mwa watu wengi imezama. Ameeleza kuwa sekta kubwa za uchumi zimo hatarini na mabenki zaidi yanaweza kuanguka na kusababisha uchumi wa Marekani uanze kurudi nyuma.Amesema hali hiyo asilani isiachiwe itokee.