Bush aita mkutano juu ya hali ya hewa
27 Septemba 2007Waziri Condoleezza Rice alitoa mwito kwa watoaji wakubwa wa gesi chafu duniani kubadilisha na kutumia nishati ambazo hazisababishi ongezeko la joto. Wakati huo huo lakini Bi Rice alisema hilo si suala la kimazingira pekee bali pia inabidi ihakikishwe kuwa uchumi utaweza kukua.
Miongoni mwa nchi zinazoshiriki katika mazungumzo haya ya siku mbili ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, China, Canada, Brazil, Mexiko, Afrika Kusini na Urusi. Mwaliko ulitolewa na rais Bush wa Marekani mwezi wa June kwenye mkutano wa nchi nane zinazoongoza kiviwanda duniani huko Heiligendamm, Ujerumani. Washiriki wanatarajiwa kuzungumzia juu ya namna ya kupunguza utoaji wa gesi chafu na kutumika teknolojia za kisasa zinazoweza kuzuia uharibifu wa mazingira pia katika nchi zinazoendelea.
Nchi kadhaa za Ulaya zina wasiwasi juu ya maslahi ya rais Bush kwenye mkutano huu. Kwa muda mrefu, Marekani imekosolewa kutochukua hatua ya maana kulinda mazingira. Marekani pia imekataa kutia saini makubaliano ya Kyoto ambayo yanaweka viwango fulani vya kupunguza utoaji wa gesi chafu kama Carbondioxide ambazo zinasababisha ongezeko la joto.
Kwa hivyo, Bush anaaminika anataka kubadilisha sifa yake na kuchukua uongozi katika suala hilo kwa kuitisha mkutano huu unaoanza leo. Akitathmini tatizo la hali ya hewa, Bush amesema hivi: “Kwanza ni kutambua kwa kweli tuna tatizo la gesi chafu zinazoharibu hali ya hewa. Pili: Tuna shida ya kutegemea mafuta. Tatu: Tunatambua kwamba inatubidi tutumie teknolojia ili kutatua tatizo hili. Na nne: Tunabeba dhamana ya kuendeleza teknolojia kama hizo na kuhakikisha zitumike pia katika nchi zinazoendelea.”
Hapo lakini Bush hakutaja kuweka masharti na malengo fulani. Bush anajulikana ana mashaka kushiriki kwenye sera za Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa. Ndiyo maana, waziri wa Ujerumani anayehusika na masuala ya mazingira, Sigmar Gabriel, kabla ya kuingia kwenye mkutano amesema: “Jukumu muhimu kabisa la Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa ujumla kwenye mkutano huu ni kumkumbusha Bush na serikali ya Marekani juu ya kauli yake pale aliposema anataka kuchukua hatua – na hatimaye anashirikiana na nchi nyingine za Umoja wa Mataifa. Vilevile inabidi tuhakikishe kuwa hatukakuwa na mbinu tofauti, bali kwamba tutafikia kwenye mazungumo ya pamoja na kupata matokeo.”
Nchi nyingine zinawatuma mawaziri wadogo au maafisa wa ngazi ya juu tu ili kuonyesha kuwa mkutano wa rais Bush haupewi umuhimu mkubwa. Umoja wa Mataifa unapanga kufanya mkutano mkubwa hapo Disemba mwaka huu huko Bali, Indonesia kwa azma ya kuweka viwango vipya vya utoaji wa gesi ya Carbondioxide kwa kipindi cha baada ya mwaka 2012 ambapo makubaliano ya Kyoto yatakapoisha.