1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yaomboleza kifo cha rais Nkurunziza

10 Juni 2020

Serikali ya Burundi imetangaza maombolezo ya kitaifa ya siku 7 kufuatia kifo cha rais wake Pierre Nkurunziza, aliyeaga dunia Jumatatu akiwa na umri wa miaka 55 kutokana na mshituko wa moyo

https://p.dw.com/p/3dYDk
Präsident Burundis Pierre Nkurunziza
Picha: Reuters/C. Guy Siboniyo

Serikali ya Burundi imetangaza maombolezo ya kitaifa ya siku 7 kufuatia kifo cha rais wake Pierre Nkurunziza, aliyeaga dunia Jumatatu akiwa na umri wa miaka 55 kutokana na mshituko wa moyo. Kulingana na katiba ya Burundi spika wa Bunge Pascal Nyabenda ndiye atakayeshika hatamu za uongozi kwa kipindi cha miezi miwili hadi atakapotawazwa Evariste Ndayishimiye aliyeibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 20 mwaka huu.

Burundi Evariste Ndayishimiye zum Sieger der Präsidentenwahl erklärt
Evariste Ndayishimiye alishinda uchaguzi wa rais Mei 20Picha: Reurters/E. Ngendakumana

Tamko la serikali kwenye Redio na Televisheni ya taifa lililosomwa na msemaji wake Prosper Ntahorwamiye ambaye pia ni Katibu mkuu wa serikali liliweka bayana kifo cha rais Nkurunziza aliyeiongoza Burundi kwa muda wa miaka 15. "Serikali ya Burundi ina masikitiko makubwa ya kuwatangazia kifo cha rais wake Pierre Nkurunziza kilichotokea Jumatatu hii kwenye Hospitali ya mkoani Karusi. Jumamosi alipokuwa akifuatilia mchezo wa mpira wa wavu kwenye uwanja wa mkoani Ngozi, rais Nkurunziza alihisi maumivu, ndipo akapelekwa kwenye hospitali ya mkoani Karusi. Baada ya kupata matibabu Jumamosi hadi Jumapili alijiskia nafuu na kuweza hata kuongea na watu walokuwa karibu naye, kabla ya Jumatatu hali yake kuwa mbaya na ndipo akakata roho. Timu ya madaktari wataalamu waliobobea walifanya kila wawezalo lakini hawakufaanikiwa. Mungu mwenye uwezo ampokee katika ufalme wake".

Serikali imetowa salamu za rambi rambi kwa familia yake huku raia wakitakiwa kusalia watulivu na kumuaga rais Nkurunziza kwa sala na maombi. Kufuatia kifo hicho  cha rais Nkurunziza serikali imetangaza msiba wa kitaifa wa siku saba kuanzia Jumanne ambapo bendera ya taifa itapandishwa nusu mlingoti. Na kwamba Utaratibu wa kufuata utatangazwa baadaye. Kifo cha rais Nkurunziza kimezusha hali ya simanzi kubwa kwa baadhi ya raia. Baadhi wakiona kuwa Nkurunziza mwenye umri wa miaka 55 alieyetambulika kama kiongozi wa kudumu milele katika chama chake, hatosahaulika. Na Raia wengine wameiambia DW Nkurunziza hatosahaulika kwa moyo wake wa uzalendo.


Kulingana na kifungu nambari 121 cha katiba, spika wa bunde Pascal Nyabenda ndiye anatakiwa kuiongoza nchi kwa kipindi cha miezi miwili hadi pale atakapotawazwa Evariste Ndayishimiye aliyeibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa mwezi jana.

Hata hivyo taarifa nyingine zinasema muhula wa bunge liliopo ulimalizika tangu April 27 ilipozinduliwa kampeni ya uchaguzi hivyo ni makamu wa rais atakayeshika hatamu. Na midhali makamu wa rais wapo wawili ni korti ya kikatiba itakao tathimini hali ilivyo na kutowa maamuzi.

Amida Issa
DW, Bujumbura