1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yalaumiwa na watetezi wa haki za binaadamu

3 Desemba 2009

Shirika la kimataifa la Haki za Binaadamu Human Right Watch, limeitaka serikali ya Burundi kupitia upya sera zake za kuwarejesha wananchi wa Rwanda ambao wamekuwa wakitafuta hifadhi ya ukimbizi nchini humo

https://p.dw.com/p/KnmL

Tarehe 27 mwezi uliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Edouard Nduwimana alitoa amri kwa jeshi la polisi nchini humo kuwarejesha makwao wanyarwanda 103 ambao waliingia nchini humo kutafuta hifadhi ya ukimbizi, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za kimataifa.

Hatua hiyo ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi, ilikuja siku chache tu baada ya ujumbe kutoka Rwanda kuiomba serikali ya Burundi kuwarejesha watu waliyokimbilia Burundi.

Inaarifiwa kuwa maafisa wa Rwanda walisema kuwa wanataka watu hao warejeshwe, ili kuonesha katika uso wa kimataifa kuwa rwanda ni nchi yenye amani kiasi kwamba hakuna watu wanaoikimbia.

Lakini Mkurugenzi wa Shirika hilo la Human Right Watch kanda ya Afrika, Georgette Gagnon amesema watu wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi wana haki ya kusikilizwa na kuangalia iwapo watakabiliwa na mateso watakaporejeshwa kwao.

Amesisitiza kuwa sheria zote za kitaifa na kimataifa zinasisitiza kuwepo kwa zingatio hilo , na kwamba nchi zote mbili Rwanda na Burundi zinawajibika kuziheshimu sheria hizo.

Watu hao 103 ni miongoni mwa mamia ya raia wa Rwanda waliyokimbilia katika majimbo ya Kirundo na Ngozi yaliyoko kaskazini mwa Burundi kati ya mwezi Julai na Septemba mwaka huu.

Shirika la Human Right s Watch Octoba mwaka huu liliwahoji wakimbizi kadhaa kutoka Rwanda kwenye mkoa wa Kirundo ambapo baadhi yao walionekana kuwa na sababu za msingi za kukimbia.

Walisema kuwa wanahofu kushtakiwa mara mbili kwa kosa moja katika mahakama za kienyeji za maridhiano na masikizano Gachacha na hofu ya kuchukuliwa na kupelekwa kusikojulikana..

Ijapokuwa kuna familia 60 zenye idadi ya watu takriban 115 ambao walisema kuwa wakimbia mapigano na kufanikiwa kuwasilisha maombi ya ukimbizi nchini Burundi, lakini wengine wakihofu kurejeshwa ,walichelewa kuwasilisha maombi yao hadi tarehe 10 mwezi uliyopita walipofanya hivyo.

Lakini Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Edouard Nduwimana aliliambia shirika hilo la kutetea haki za binaadam kwamba maombi ya kundi hilo la wakimbizi kutaka hifadhi, yalichelewa kuwasilisha, na kwamba ni lazima warejeshwe Rwanda.

Aliongeza kuwa hakuna tena maombi mapya ya ukimbizi yatakayopokelewa na kusisitiza kuwa wanawachukulia watu hao kama ni watu waliyoingia nchini Burundi kinyume na sheria.

Wakati huo huo Shirika la habari Agence Burundaise de la Press liliripoti kwamba kiasi ya Wanyarwanda 70 waliotafuta hifadhi na ambao walikuwa wakijificha majumbani miongoni mwa jamii ya Vumbi, Ntega na Marangara kwa miezi kadhaa walijaribu kuomba hifadhi tarehe 10 mwezi uliopita. Wengi hawakujitokeza kwa kuhofia watarejeshwa kwao mara moja.

Burundi ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba wa kimataifa wa 1951 kuhusiana na wakimbizi, ambao unazuia nchi moja kuwarejesha wakimbizi katika nchi waliyotoka, pindi uhuru na usalama wao utakua hatarini.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Humar Rights Watch report

Mhariri:Mohamed Abrul-Rahman