1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBurkina Faso

Burkina Faso yawatafuta wanawake 50 waliotekwa

17 Januari 2023

Maafisa wa usalama Burkina Faso wanaendelea na juhudi za kuwatafuta takriban wanawake 50 waliotekwa nyara na washukiwa wanamgambo wa Jihad.

https://p.dw.com/p/4MHlr
Benin | Fotoreportage Marco Simoncelli aus Porga
Picha: Marco Simoncelli/DW

Maafisa wa usalama wanaendelea kuwatafuta takriban wanawake 50 waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye misimamo mikali ya Kiislamu katika jimbo linalozongwa na machafuko ya wanamgambo kaskazini mwa Burkina Faso. Gavana wa jimbo hilo Luteni Kanali Rodolphe Sorgho amesema.

Wanawake hao walitekwa nyara katika matukio mawili tofauti siku ya Alhamisi na Ijumaa, walipokuwa wakitafuta matunda msituni. Hilo ni shambulizi la hivi karibuni zaidi linaloshukiwa kufanywa na wanamgambo wanaohusishwa na mtandao wa Al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Miili 28 ya watu waliouwawa yapatikana Burkina Faso

Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk ametaka wanawake hao kuachiwa huru mara moja bila masharti. Amewahimiza maafisa wa serikali kuwakamata waliohusika na kuhakikisha wameadhibiwa.

Luteni Kanali Rodolphe Sorgho, gavana wa jimbo la Sahel amesema kupitia taarifa kwamba punde tu ripoti ya kutoweka kwao ilipotolewa, juhudi zilianzishwa kuwatafuta ili wapatikane wakiwa salama. Ameongeza kuwa wanawake wengine walifaulu kutoroka na ndio walitoa taarifa kwa vyombo vya usalama.

Hofu yaibuka kuwa wanamgambo waanza kuwalenga wanawake Burkina Faso

"Mbinu zote zilizopo zinatumika, angani na ardhini, ili kuwapata wanawake hao,” afisa mmoja aliliambia shirika la habari la AFP.

Kisa hicho kimezusha hofu miongoni mwa wanaharakati wa haki za binadamu. Dauda Diallo ambaye ni Katibu wa kundi la kupambana na uhalifu wa kiholela na unyanyapaa katika jamii, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kile amekitaja kuwa 'hali mpya'.

Burkina Faso ni miongoni mwa nchi maskini na vilevile yenye machafuko zaidi ulimwenguni.
Burkina Faso ni miongoni mwa nchi maskini na vilevile yenye machafuko zaidi ulimwenguni.Picha: Olympia de Maismont/AFP/Getty Images

"Hii ni mara ya kwanza tunashuhudia utekaji nyara wa idadi kubwa ya wanawake. Wakati mwingine tulirekodi visa vichache, lakini wanawake waliweza kutembea maeneo mengi kuliko wanaume. Lakini leo, hali hii inatia wasiwasi, na ni kana kwamba hii ni hali mpya katika masuala ya usalama ambayo lazima tuzingatie,” Amesema Diallo.

Mataifa ya ukanda wa Sahel bado yanahangaishwa na uasi

Burkina Faso ni miongoni mwa nchi maskini na vilevile yenye machafuko zaidi ulimwenguni.

Tangu 2015, nchi hiyo imekuwa ikizongwa na uasi na mashambulizi ya wanamgambo wa kidini, hali ambayo imesababisha vifo vya maelfu na kuwalazimisha takriban watu milioni mbili kuyakimbia makaazi yao.

Uasi na machafuko ya wanamgambo Burkina Faso

Eneo la tukio hilo limekuwa likizingirwa na makundi ya wanamgambo na pia limekuwa likitegemea chakula kutoka nje.

Turk kwenye taarifa yake amesema, huenda hii ni mara ya kwanza kutokea shambulizi kama hilo linalonekana kuwalenga wanawake moja kwa moja nchini Burkina Faso.

Wanajeshi wa Burkina Faso Na Mali wakutana kujadili usalama

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa usalama katika jeshi la Burkina Faso ambaye alizungumza kwa sharti la kutotambulishwa jina, amesema kutoweka kwa wanawake hao ni kisa cha kwanza cha utekaji nyara wa idadi kubwa ya wanawake tangu mgogoro wa usalama uanze nchini humo. Ameongeza kuwa kila hatua sharti ichukuliwe ili kuzuia mkasa kama huo kutokea tena.

Ufaransa ambayo ni mshirika wa karibu wa Burkina Faso na pia mkoloni wake wa zamani, imeulaani utekaji huo na kutaka wanawake hao waachiliwe huru mara moja.

(Chanzo: AFPE)