Burhan aapa kuvimaliza vita muda mfupi ujao
28 Agosti 2023Burhan alisema siku ya Jumatatu (Agosti 28) akiwa katika mji wa Port Sudan kwamba hakuna aliyemsaidia kutoka kwenye makao makuu ya jeshi na wala haikutokana na makubaliano yoyote, bali ilikuwa ni operesheni ya kijeshi yenye mafanikio.
Soma zaidi: RSF iko tayari kuweka silaha chini na kufanya mazungumzo na jeshi la Sudan
Alisema wanahamasisha kila mahali kuuangusha uasi huo uliofanywa na mamluki wanaotoka maeneo mbalimbali ulimwenguni.
"Hakuna tena muda wa majadiliano, bali kwa sasa tunaelekeza nguvu zote kwenye vita ili kuuhitimisha uasi huu," alisema jenerali huyo kwenye ziara yake ya kwanza nje ya makao makuu ya jeshi tangu mwezi Aprili yalipoanza mapigano.
Burhan alitoa matamshi hayo siku moja baada ya kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, kuchapisha taarifa yenye mapendekezo 10 ya kuvimaliza vita na kujenga kile alichokiita "Sudan Mpya."