Bunge Uganda lafungwa kutokana na corona
23 Juni 2021Kulingana na taarifa iliyotolewa na naibu katibu wa bunge Henry Waiswa, wabunge wote na wafanyakazi wa bunge watakwenda likizo ya wiki mbili. Kipindi hicho kimeelezwa kwenda sambamba na kile cha zuio walilowekewa raia wengine ili kudhibiti kasi ya maambukizi ya COVID-19 ambayo kwa sasa inaelezewa kuwa kwa kiwango cha asli mia 17 nchini Uganda. Hii ina maana kuwa kati ya watu mia moja, 17 wana COVID-19. Hata hivyo, usimamizi wa bunge umekanusha taarifa zilizochapishwa katika gazeti moja kwamba wabunge 200 ndiyo wanaugua COVID-19.
Kile ambacho kimewakera wananchi wengi ni kwamba taasisi kuu za serikali kama bunge zimendelea na shughuli zao licha ya wengine kufungiwa ili kuepusha mikusanyiko inayoweza kusababisha maambukizi ya COVID-19. Lakini kiranja wa upinzani bungeni John Baptist Nambeshe anaelezea kuwa mazingira yao ya kukutana ni salama.
Jumatatu wiki hii, shughuli nyingine ya kuapishwa kwa baraza la mawaziri ilifanyika na kuwaleta pamoja zaidi ya mawaziri 80, familia zao waliokuja kushuhudia tukio hilo la kihistoria kwao, walinzi pamoja na wandishi habari. Ila mawaziri 17 wateule hawakuhudhuria pamoja na spika mpya wa bunge Jacob Oulanya. Ilibainika mawaziri hao pia wanaugua COVID-19. Hata hivyo afisa wa bunge Jane Kibirige aliyesimamia hafla hiyo iliyohudhuriwa na rais Museveni alidokeza kuwa haingeahirishwa kwa sababu ni muhimu ili serikali iweze kuendelea na shughuli zake.
Kulingana na takwimu za sasa za wizara ya afya, Uganda imesajili wagonjwa 73,409 wa COVID-19. Lakini siku ya jana pekee ya Jumanne, watu 722 waligunduliwa kuwa na COVID-19. Watu 34 wametajwa kufariki kutokana na ugonjwa huo hapo jana.
Lubega Emmanuel DW Kampala