1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Tanzania lamfurusha bungeni Godbless Lema

Sylvia Mwehozi
4 Aprili 2019

Mbunge wa jimbo la Arusha, Tanzania kupitia chama kikuu cha upinzani CHADEMA, Godbless Lema amesimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia siku ya Alhamis.

https://p.dw.com/p/3GEun
Tansania Parlament Dodoma - Parlamentsvorsitzende mit Philip Mpango und Premierminister Kassim Majaliwa
Picha: DW/S. Khamis

Akisoma taarifa ya kamati ya kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge katika kikao cha tatu cha bunge la Tanzania linaloendelea hivi sasa hapa mjini Dodoma, mwenyekiti wa kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka, amesema kamati yake imejiridhisha pasina shaka kuwa mbunge Godbless Lema amelidharau na kulidhalilisha bunge kwa kusema kuwa anaunga mkono kauli ya Mkaguzi na Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Profesa Mussa Assad kuwa bunge la Tanzania ni dhaifu na hivyo kamati hiyo baada ya kusikiliza shauri lake limemkuta na hatia na kisha kuazimia mbunge huyo apewe adhabu ya kutohudhuria mikutano mitatu ya bunge.

Hata hivyo, hatua ya kumkuta Lema na hatia ya kulidharau na kulidhalilisha bunge, imepokelewa kwa hisia tofauti na wabunge John Mnyika wa CHADEMA na Mariam Kisangi kutoka chama tawala cha CCM wakati wakichangia taarifa hiyo ya kamati ya maadili.

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ametoa onyo kwa mbunge Lema kuwa wakati huu akitumikia adhabu yake hapaswi kutoa kauli zitakazovunja hadhi na heshima ya bunge, vinginevyo ataendelea kukiona cha mtemakuni na atarudishwa tena katika kamati ya maadili. Mkutano huo wa 15 wa bunge la Tanzania utaendelea na kikao chake cha tatu siku ya Ijumaa.