1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge lashinikiza kuhodhi mchakato wa Brexit

25 Machi 2019

Wabunge wa bunge la Uingereza huenda wakapata ushindi katika kura hii leo ya kushinikiza bunge hilo kuchukua udhibiti wa mchakato wa nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya ama Brexit kutoka kwa serikali

https://p.dw.com/p/3FdNd
Großbritannien London - Parlamentssitzung
Picha: picture-alliance/AP Photo/UK Parliament/M. Duffy

Bunge hilo linapiga kura kujaribu kutafuta wingi wa njia mbadala ya kusonga mbele kwa kuondoa mkwamo uliolikumba bunge hilo. 

Chanzo kimoja cha serikali kimesema mabadiliko yaliyopendekezwa na wabunge wa vyama tofauti yaliyoongozwa na mbunge wa chama cha Kihafidhina cha waziri mkuu Theresa May Oliver Letwin, yanataka kubadilishwa kwa sheria za bunge ifikapo Machi 27 ili kutoa muda kwa wabunge kujadiliana na kupiga kura kuhusu njia mbadala za kusonga mbele. 

Serikali inataraji hatua hiyo kupitishwa na bunge, ambayo kulingana na chanzo hicho huenda mwisho wake ikailazimisha serikali kufanyia kazi mapendekezo yoyote yale ambayo yanaweza kuwashawishi wabunge wengi katika bunge lililogawanyika kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa masuala ya biashara ya kimataifa Dr. Liam Fox amesema mpango wa Brexit hautapitishwa kutasababisha kile alichokitaja kama "usaliti mkubwa" wa imani ambayo bunge liliweka kwa raia waliopiga kura ya maoni.

UK Brexit | Internationaler Handelsminister Liam Fox im Unterhaus
Waziri wa mahusiano ya kimataifa wa Uingereza, Liam Fox ameonya kuhusu usaliti kwa wapiga kura iwapo Brexit itashindikana.Picha: picture-alliance/empics/PA Wire

"Tunatakiwa kuendelea kuwaeleza wabunge machaguo iwapo watakataa kuyapitisha makubaliano ya May. Machaguo hayo ni ama kuondoka bila ya makubaliano au kutoondoka kabisa Umoja wa Ulaya. La kwanza litakuwa gumu kwa sababu bunge limeweka wazi kwamba halitaki kuondoka bila ya makubaliano. Na ninadhani kutoondoka Umoja wa Ulaya kutakuwa ni usaliti mkubwa kwa wapiga kura ya maoni." alisema Fox.

 Umoja wa Ulaya tayari umekamilisha maandalizi ya Uingereza kuondoka bila ya makubaliano.

Msemaji wa waziri mkuu May amesema serikali ya Uingereza inaweza tu kupiga kura nyingine aliyoiita yenye maana juu ya mpango wa May wa Brexit iwapo itapata nafasi ya ungwaji mkono wa bunge itakapouwasilisha katika jaribio lake la tatu.

EU-Gipfel Brexit in Brüssel | Theresa May
Waziri mkuu Theresa May bado anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka bungeni akitakiwa kujiuzuluPicha: AFP/E. Dunand

Serikali huenda ikatakiwa kuwasilisha mezani mpango wa dharura kabla ya kukamilika kwa shughuli za bunge siku ya Jumatatu na hatimaye kupigwa kwa kura hiyo siku ya Jumanne. Msemaji huyo amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali itarejesha mchakato huo wa kura iwapo tu itakuwa na imani kwamba itakuwa katika nafasi ya kushinda. Hata hivyo alikataa kusema iwapo kura hiyo itapigwa siku ya Jumanne.  

Msemaji huyo, amesema baraza la mawaziri lililokutana hii leo halikujadili kuhusu mustakabali wa May. Baadhi ya wabunge walimtaka May kutaja tarehe atakayoondoka, wakisema kuwa ndio matokeo ya kuukubali mkataba huo wa Brexit.

Katika hatua nyingine, tume ya Umoja wa Ulaya nayo imetangaza hii leo kukamilisha maandalizi ya Uingereza kuondoka kwenye Umoja huo bila ya makubaliano, katika wakati ambapo wasiwasi wa taifa hilo kuondoka bila ya makubaliano kati yao ukizidi kuongezeka.

Tume hiyo imeelezea hatua itakazochukua kwenye maeneo 13, kuanzia sheria za usafiri wa anga na barabara hadi kanuni za usafirishaji, haki za uvuvi na hata shughuli za kibenki, huku ikisisitiza kwamba huenda hiyo ikapunguza vurugu lakini si kuzuia kabisa.  

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo