1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge lampa idhini Putin kutuma vikosi Crimea

2 Machi 2014

Rais Vladimir Putin wa Urusi amepewa idhini ya bunge kutuma jeshi la nchi hiyo Ukraine hatua ambayo amesema inahitajika ili kuwalinda watu wenye asili ya Urusi na wafanyakazi wa kambi ya kijeshi ya Urusi huko Crimea.

https://p.dw.com/p/1BI1V
Mwanajeshi akisubiri wakati magari ya kijeshi yakiwa nje ya kituo cha mpaka cha Ukraine cha Balaclava katika jimbo la Crimea(01.03.2014).
Mwanajeshi akisubiri wakati magari ya kijeshi yakiwa nje ya kituo cha mpaka cha Ukraine cha Balaclava katika jimbo la Crimea(01.03.2014).Picha: Reuters

Ombi la Putin lilidhinishwa kwa kauli moja sasa itategemea rais kuamuwa wakati gani kuitumia haki hiyo aliyopewa.

Spika wa bunge Valentina Matviyenko pia ameiagiza kamati ya mambo ya nje ya bunge kumtaka Putin kumrudisha nyumbani balozi wake kutoka Marekani.

Putin amesema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Urusi Kremlin kwamba anawasilisha ombi la kutumia wanajeshi wa ulinzi wa Shirikisho la Urusi katika ardhi ya Ukraine hadi hapo hali ya kijamii na kisiasa nchini humo itakapokuwa katika hali ya kawaida.Kwa mujibu wa katiba ya Urusi inabidi bunge liidhinishe hatua hiyo.

Huko Crimea waziri mkuu wa jimbo hilo mwenye kuiunga mkono Urusi awali alidai udhibiti wa jeshi na polisi kwenye jimbo hilo na alimtaka Putin amsaidie kudumisha amani na kuzidi kuuchochea mzozo huo baina ya nchi hizo mbili jirani.

Mzozo wapamba moto upya

Huku ni kupamba moto upya kwa mzozo huo kufuatia kuondolewa madarakani kwa rais wa Ukraine aliyekuwa akiiunga mkono Urusi wiki iliopita na vuguvugu la waandamanaji lenye nia ya kuielekeza Ukraine kwenye Umoja wa Ulaya na kujitenga na Urusi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: DW/B. Riegert

Watu wenye silaha walioelezewa kuwa ni vikosi vya Urusi walividhibiti viwanja vikuu vya ndege na kituo cha mawasiliano huko Crimea hapo Ijumaa. Ukraine ilishutumu Urusi kwa kufanya uvamizi na kulikalia na kwa mabavu jimbo hilo madai ambayo yameleta sura mpya ya kutisha kwa mzozo huo na kuzusha hofu kwamba Urusi inachukuwa hatua za kuingilia kati kijeshi katika rasi hiyo yenye umuhimu kimkakati ambapo meli za kivita za Urusi zina kambi yake katika Bahari Nyeusi.

Wananchi wagawika

Wananchi wa Ukraine wamegawika katika suala la uaminifu kati ya Urusi na Ulaya ambapo Ukraine ya magharibi wanapigania mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya wakati mikoa ya mashariki na kusini ikitegemea msaada wa Urusi.Jimbo la Crimea lina wakaazi wengi wanaozungumza Kirusi.

Wafuasi wa Urusi katika maandamano katika mji mkuu wa Crimea- Simferopol. (01.03.2014).
Wafuasi wa Urusi katika maandamano katika mji mkuu wa Crimea- Simferopol. (01.03.2014).Picha: Sean Gallup/Getty Images

Waziri Mkuu wa Crimea Sergei Aksyonov ametangaza kwamba majeshi ya ulinzi, polisi, wapelelezi wa taifa na walinzi wa mipakani katika jimbo hilo watawajibika kwa amri zake tu.

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk ameufunguwa mkutano wa baraza la mawaziri katika mji mkuu wa Kiev kwa kutowa wito kwa Urusi kutotia chokochoko huko Crimea rasi ilioko katika Bahari Nyeusi.

Amekaririwa na shirika la habari la Urusi Intefax akisema "Tunatowa wito kwa serikali na maafisa wa Urusi kuviita vikosi vyao na kuvirudisha kambini". Ameongeza kusema "Washirika wa Urusi acheni kuchochea uasi wa kiraia na kijeshi nchini Ukraine."

Hali ya wasi wasi

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema amekuwa na wasiwasi jinsi mambo yanaevyoendelea katika jimbo hilo la Crimea nchini Ukraine. Akizungumza katika hotuba yake aliyoitoa katika tukio la kitamaduni mjini Berlin Jumamosi Merkel amesema mambo yanayotokea Ukraine yanawawatia mashaka na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya mipaka ya Ukraine.

Wanajeshi wakilinda jengo la bunge la Crimea. (01.03.2014).
Wanajeshi wakilinda jengo la bunge la Crimea. (01.03.2014).Picha: Sean Gallup/Getty Images

Kwa mujibu wa wanadiplomasia waandamizi wa Ulaya yumkini Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton akaitisha mkutano mpya wa dharura wa Umoja wa Ulaya pengine hata Jumatatu kujadili hali ya Ukraine.

Mkutano huo utakuwa wa pili kuhusu mzozo wa Ukraine kufanywa na wakuu wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya wa nchi wanachama 28 katika kipindi kisichozidi wiki mbili baada ya kukubaliana katika mkutano wa dharura wa Februari 20 kuwawekea vikwazo maafisa wa utawala wa Yanukovich wanaonekana kuhusika na vifo na ukandamizaji wa wapinzani mitaani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Sudi Mnette