Bunge la Zimbabwe kuidhinisha Marekebisho ya Katiba leo.
5 Februari 2009Hatua hiyo ya bunge kuidhinisha mswada huo wa marekebisho ya katiba leo, inafuatia uamuzi uliotolewa na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika, SADC, mwezi uliopita, kwamba leo iwe ni siku ya mwisho kwa bunge kuidhinisha mswada huo wa marekebisho ya katiba kuruhusu kuundwa kwa serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa.
Marekebisho hayo ya katiba yatahusisha pia kuundwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu, ambayo inatarajiwa kuchukuliwa na kiongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change MDC, Morgan Tsvangirai.
Majadiliano kuhusiana na mabadiliko hayo, yaliahirishwa jana, ili kutoa muda zaidi kwa wajumbe kuweza kuzungumzia masuala yaliyobaki.
Mapema leo chama cha upinzani MDC, kiliripoti kuwepo maendeleo katika mashauriano hayo ya kumaliza tofauti yao na chama tawala kinachoongozwa na rais Robert Mugabe, cha UANU-PF, ili kuweza kuunda serikali ya pamoja, baada ya mazungumzo ya pande hizo mbili yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Msemaji wa chama cha MDC, Nelson Chamisa, amesema wapatanishi kutoka chama chake na chama tawala cha ZANU- PF, walijadiliana kuhusiana na mgawanyo wa wizara nyeti, suala ambalo ndio kikwazo kikuu katika kutekeleza makubaliano hayo ya kuunda serikali ya pamoja.
Aidha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC- ilipanga pia February 11, iwe ni siku ya mwisho ya kuapishwa kwa Morgan Tsvangirai kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, huku mawaziri na manaibu wao wakiwa wamepangiwa kuapishwa Februari 13.
Wakati huo huo, kesi ya uhaini inayomkabili naibu kiongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe, MDC, bwana Tendai Biti imepangwa kusikilizwa Mei 4 mwaka huu.
Tendai Biti, mwanasheria na katibu mkuu wa chama hicho anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutaka kumpindua madarakani rais wa nchi hiyo Robert Mugabe.
Anashutumiwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyozua utata mnamo mwezi Machi mwaka uliopita, kabla ya tume ya uchaguzi nchini humo kutoa rasmi matokeo hayo, na pia kwa kutayarisha nyaraka zinazoaminika kuwa ni njama za kupindua serikali ya rais Mugabe, kupitia wizi wa kura.
Hata hivyo uamuzi wa kimahakama unatarajiwa kutolewa Ijumaa, kama Tendai Biti atawekwa rumande.
Tendai Biti ambaye alichaguliwa mwaka uliopita kuwa mbunge wa jimbo la Harare, ni kiongozi wa ujumbe wa chama cha upinzani cha MDC, kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai, katika mazungumzo ya kupatikana muafaka wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na chama tawala nchini humo cha ZANU-PF.