1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani lauunga mkono mpango wa Kansela Merkel

17 Oktoba 2008

Ni hatua ya kukabiliana na atahri msukosuko wa fedha duniani.

https://p.dw.com/p/Fbsz
Kansela Merkel akifafanua juu ya mpnago wake bungeni.Picha: AP

Kwa wingi mkubwa bunge la Ujerumani leo limeuidhinisha mpango wa Kansela Angela Merkel kuiokoa sekta ya Benki. Mpango huo wa euro bilioni 480 unalenga katika kushajiisha imani ya wawekezaji wa kimataifa, baada ya majuma kadhaa ya msukosuko katika masoko ya hisa.

Mpango huo ulipitishwa kwa wingi mkubwa wa vyama vya CDU na SPD vinavyounda serikali ya Muungano na pia FDP wa jumla ya kura 476,pamoja na kupingwa kwa kura 99 za wabunge wa chama cha kijani Grüne na kile cha mrengo wa shoto Linke. Hatua hiyo inafuatiamakubaliano hapo jana na mawaziri wakuu wa mikoa na sasa inatarajiwa mno kwamba baraza la mabunge ya mikoa Bundesrat litauidhinisha pia baadae leo, ili uanze kufanya kazi.

Kansela Merkel aliuzindua mpango huo Jumatatu kama sehemu ya juhudi za serikali duniani kuyatuliza masoko ya hisa na kuzisaidia taasisi za fedha kukabiliana na msukosuko huo ulioibuka mwaka jana kutokana na kuanguka kwa biashara ya ununuzi wa nyumba nchini Marekani.

Lakini akizungumza bungeni mjini Berlin leo, Waziri wa uchumi Michael Glos alisisitiza kwamba mpango huo wa serikali una lengo la kuwalinda raia kuliko wenye mabenki, na akasema hakuna haja ya kuwa na wasi wasi juu ya mtazamo wa uchumi wa Ujerumani, lakini knyume chake alisema Waziri Glos," tunaweza kuyatatua matatizo hayo."

Akichangia katika mjadala kabla ya kupigwa kurea kiongozi wa wabunge wa SPD bungeni Peter Struck alitoa wito wa suhirikiano kulitatua tatizo hilo,"Hatuna budi hivi sasa kuachana na mabishano na kusimama pamoja kwa mshikamano kulitatua kwa busara tatizo hili."

Mpango huo wa serikali unahusika na hatua kadhaa kama hakikisho la dhamana kwa upande wa serikali, kusaidia kupunguza athari kwa mabenki zinazotokana na kubanwa kwa mikopo pamoja na hatua za kuzipa tena mtaji taasisi za fedha.

Hata hivyo wadadisi wameonya kwamba mpango huo wa Ujerumani ulioungwa mkono na bunge, huenda ukashindwa kuuokoa uchumi wake ulio mkubwa barani Ulaya , iwapo msukosuko wa fedha utazidi kuendelea kote duniani.

Serikali bado haijafafanua ni mabenki gani yanayohitaji kunusuriwa, lakini benki 9 zinazomilikiwa na mikoa ndizo zinazoonekana kuwa dhaifu .

Mengi miongoni mwa mataifa ya kanda ya nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya euro, kuwa na mipango inayofanana kila mmoja ukiwa na kitita kikubwa cha fedha kama dhamana kwa mikopo ya mabenki yao pamoja na utaifishaji nusu wa baadhi ya tasisi za fedha.