1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani laukumbuka mwaka wa mia moja tokea kuanza vita kuu vya kwanza

Abdu Said Mtullya5 Julai 2014

Bunge la Ujerumani leo limeukumbuka mwaka wa mia moja baada ya kuanza vita kuu vya kwanza na kwa ajili hiyo Spika wa Bunge hilo Norbert Lammert ametoa mwito wa kuitatua mizozo ya dunia kwa njia ya mazungumzo.

https://p.dw.com/p/1CVPt
Wabunge wa Ujerumani wakumbuka kuanza kwa vita kuu vya kwanza miaka mia moja iliyopita
Wabunge wa Ujerumani wakumbuka kuanza kwa vita kuu vya kwanza miaka mia moja iliyopitaPicha: picture-alliance/dpa

Spika wa Bunge la Ujerumani.Lammert amesema matumizi ya nguvu za kijeshi ,kimsingi siyo njia mwafaka kisiasa, katika kuyaleta mabadiliko yanayokusudiwa . Spika Nobert Lammert ameshauri kwamba, ikiwa ni lazima kabisa, nguvu za kijeshi zitumike kama njia ya mwisho katika kuitatua migogoro.

Akisisitiza umuhimu wa amani duniani, katika kumbumbuku iliyohudhuriwa pia na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Spika Nobert Lammert alieleza kwamba Wajerumani walikuja kujua baadae sana kwamba nguvu za kijeshi siyo njia mwafaka katika juhudi za kuyaleta mabadiliko ya kisiasa ambayo jamii inayadhamiria.

Haki ya kugoma kulitumikia jeshi imo katika katiba

Hata hivyo amesema Ujerumani ni nchi ya kwanza duniani,kuingiza katika katiba yake uamuzi wa mtu wa kupinga kulitumikia jeshi kwa shabaha za kivita ,kuwa haki ya kimsingi" Ujerumani pia ni nchi ambapo Bunge ndilo lenye mamlaka ya kutoa kauli ya mwisho kuamua juu ya vita.

Spika wa Bunge la Ujerumani bwana Lammert amesema vita vya kwanza vya dunia vilikuwa kama upepo mbaya uliopeperusha maradhi katika karne ya 20. Hata hivyo amesema tofauti na hali ya miaka ya vita kuu vya kwanza, leo hakuna mtu anaetaka vita, licha ya matukio ya nchini Ukraine.

Vita Kuu vya kwanza vilikuwa vita vya mwisho vikubwa ambapo silaha za kawaida zilitumika lakini wakati huo vilikuwa vita vya kisasa. Vita hivyo vilivyoanza mnamo mwaka 1914 hadi 1918 vilisababisha vifo vya mamilioni ya binadamu duniani. Mabadiliko makubwa ya nyakati yalianza kutokana na vita hivyo. Ushawishi wa nchi za Ulaya katika siasa za dunia ulianza kupungua na hatimaye kumalizika.

Wajerumani wawapinga Hitler na Stalin

Mgeni rasmi kwenye kumbukumbu ya miaka 100 ya vita vikuu vya kwanza,iliyofanyika kwenye Bunge la Ujerumani, alikuwa mtaalamu wa siasa mwenye nasaba za kifaransa na kijerumani Alfred Grosser aliesema kuwa Ujerumani ni nchi mahsusi.

Ameeleza kuwa Ujerumani ni nchi iliyomkataa Hitler katika wakati uliotangulia na ilimkataa kiongozi wa Urusi dikteta Stalin katika wakati uliofuatia. Hata hivyo mtaalamu huyo wa masuala ya siasa Grosser ameeleza kuwa Ujerumani ndiyo nchi iliyoathirika mno kutokana na vita .Hadi miaka ya karibuni Ujerumani ilikuwa inabebeshwa lawama juu ya kuanza vita zote mbili kuu.

Mwandishi Marx,Bettina

Tafsiri:Mtullya Abdu.

Mhariri: