1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani laridhia askari zaidi Afghanistan

Abdu Said Mtullya26 Februari 2010

Ujerumani imeamua kuongeza idadi ya wanajeshi wake wanaolinda amani nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/MDP6
Wanajeshi wa Ujerumani wakitoa mafunzo kwa askari na polisi wa Afghanistan.Picha: dpa

Bunge la Ujerumani limepitisha kwa kura nyingi uamuzi wa kuongeza wanajeshi nchini Afghanistan kutoka 4500 hadi 5350.

Wabunge 429 kati ya 586 waliupitisha uamuzi huo .Wanajeshi hao, ambao ni sehemu ya majeshi ya kimataifa ISAF,watakuwapo nchini Afghanistan kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.

Hata hivyo, palikuwa na patashika kubwa bungeni wakati wa mjadala kutokana na upinzani mkali wa chama cha mrengo wa shoto, "The Left Party". Wabunge wa chama hicho waliinua juu mabango yaliyoandikwa majina ya raia wa Afghanistan waliouawa katika shambulio la ndege katika mji wa Kundus.

Sokomoko lilikuwa kubwa kiasi kwamba Spika wa bunge, Nobert Lammert, alilazimika kuwatoa nje wabunge hao wa chama cha mrengo wa shoto.Wabunge wa chama hicho, kimsingi, wanapinga kuwepo majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan.

Akifafanua msimamo huo, mbunge wa chama hicho, Christiane. Buchholz alisema mkutano wake na jamaa wa wahanga wa shambulio ulimfanya abaini wazi kwamba Ujerumani imo vitani dhidi ya watu wa kawaida wa Afghanistan.

Katika shambulio hilo, raia 142 wa Afghanistan waliuawa baada ya ndege za Nato kulipiga lori la tanki la petroli.

Kamanda wa jeshi la Ujerumani aliamuru shambulio hilo.

Baada ya wabunge wa chama cha mrengo wa shoto kutolewa nje, bunge liliendelea na kikao na kupiga kura.

Hata hivyo mbunge wa chama kingine cha upinzani, alimlaumu spika kwa hatua ya kufukuzwa bungeni kwa wabunge wa chama cha mrengo wa shoto.Mbunge huyo bwana Hans Christian Ströbele amesema hatua hiyo itatoa ishara mbaya kwa watu wa Afghanistan na duniani kote.

Uamuzi wa kuongeza askari nchini Afghanistan umeungwa mkono na vyama vilivyomo katika serikali ya mseto-CDU,CSU na cha Waliberali-FDP.

Chama cha upinzani cha SPD pia kimeunga mkono uamuzi wa kupeleka wanajeshi zaidi lakini kinataka pawepo uwazi juu ya ratiba ya kuondolewa majeshi ya Ujerumani kutoka Afghanistan.

Mwandishi: Bettina Marx/Mtullya/ZR

Mhariri: Miraji Othman