1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani kufanya kikao chake cha kwanza

Sekione Kitojo
24 Oktoba 2017

Wolfgang Schaeuble, waziri wa zamani wa fedha wa Ujerumani mwenye dhamira ya chuma, anatarajiwa kuwa spika mpya wa bunge, akisafisha njia ya mabadiliko makubwa ya madaraka katika taifa  lenye uchumi mkubwa barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/2mOR5
Wolfgang Schäuble CDU
Wolfgang Schäuble wa CDU kuwa spika mpya wa BundestagPicha: picture-alliance/dpa/M.Kappeler

wabunge  wa  Ujerumani  wanafanya  kikao  cha  kwanza  cha  bunge leo Jumanne, baada  ya  vyama  vya  kihafidhina  vinavyoongozwa na  kansela  Angela  Merkel  kuibuka na  ushindi  lakini  pii wakiwa hoi katika  uchaguzi  mkuu  wa  mwezi  Septemba, ambao chama cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  kilishinda  viti kwa  mara  ya kwanza.

Washington Schäuble
Wolfgang Schaueble anayetarajiwa kuwa spika mpya wa bunge la Ujerumani BundestagPicha: Imago/photothek/T. Koehler

Kikao  cha  leo  kitashuhudia  bunge lenye  viti 709 likimchagua spika  wa  bunge, ambapo  waziri  wa  fedha  anyeondoka  katika wadhifa  huo  Wolfgang Schaeuble  mwenye  umri  wa  miaka  75 , na  mbunge  aliyelitumikia  bunge  kwa  muda  mrefu  wa  miaka  45 nchini  humo, akitarajiwa  kuchukua  nafasi  ya Norbert Lammert.

Haifahamiki  nani  atachukua  wadhifa  wa  makamu  spika , wakati upande  wa  chama cha  siasa  za  wastani  za  mrengo  wa  kushoto cha  Social Democratic SPD , ambacho  kitakuwa  upande  wa upinzani  kwa  mara  ya  kwanza  baada  ya  muda  wa  miaka minne, kikitafakari  kuwateua  wagombea  ambao  ni  pamoja  na kiongozi  wa  zamani  wa  kundi  la  wabunge  wa  chama  hicho bungeni Thomas Oppermann na  waziri  wa  zamani  wa  afya  Ulla Schmidt.

Norbert Lammert Bundestagspräsident
Spika wa Bundestag anayeondoka madarakani Norbert LammertPicha: picture-alliance/AA/M. Gambarini

Chama  cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  cha  Alernative for Germany AfD, ambacho  kimepata  viti 94 katika  bunge  hilo  jipya baada  ya  kupata  asilimia  13  ya  kura, kimempendekeza  Albrecht Glaser  kuwa  makamu  wa  spika.

Glaser huko  nyuma  amewahi  kushambuliwa  kutokana  na  taarifa za  utata  kuhusiana  na  Uislamu.

Makabiliano makali

Chama  hicho  cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  cha  AfD kinatarajiwa  kukabiliana  vikali  na  vyama  vingine  kutokana  na uamuzi  wake  wa  kumteua  mgombea  huyo  wakati  kikao kitakapoanza leo.

Berlin Bundestagssitzung Totale
Bunge la Ujerumani BundestagPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Katika  kikao  hicho  cha  leo  cha  Bundestag , Wolfgang Schaeuble anaweza kutarajia  uungwaji  mkono  mkubwa  na  kuteuliwa  kuwa spika  wa  bunge. Baadaye  wabunge  watapiga  kura  kuwachagua makamu  sita  wa  spika , mmoja  kutoka  kila  chama kinachowakilishwa  bungeni.

Uteuzi  wa  makamu  wa  spika  wa  chama  cha  AfD , ambae  ni Albrecht Glaser , mwenye  umri  wa  miaka  75, unaleta  utata baada ya  kiongozi  huyo kutoa maelezo ya  kuukashifu  Uislamu  kwamba ni  nadharia  ya  kisiasa  badala  ya  dini , na  kusema  Waislamu hawapaswi  kupewa  haki  ya  uhuru  wa  kidini  kwa  kuwa  Uislamu hauheshimu  uhuru  huo.

Deutschland AfD Bundesparteitag in Stuttgart Albrecht Glaser
Albrecht Glaser wa chama cha AfDPicha: picture alliance/dpa/C. Schmidt

Chama  cha  Social Democrats , SPD, kile  cha  Kijani , Greens, chama  kinachopendelea  wafanyabiashara  cha  Free Democrats FDP na  kile  kinachoelemea  zaidi  siasa  kali  za  mrengo  wa kushoto  cha Left Party  vimezungumzia  kupinga  uteuzi  wa  Glaser.

Andrea Nahles , kiongozi wa  chama  cha  Social democrats  bungeni , amekiambia  kituo cha  televisheni  cha  ZDF kwamba  glaser ameshindwa  kusahihisha matamshi  yake kuhusu  Uislamu, hali inayokwenda  kinyume na  haki  ya  uhuru  wa  kuabudu  nchini Ujerumani, na  kutupilia mbali  ombi  lake  la  kutaka  mjadala  kuwa ni  kichekesho.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae /

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman