1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ufaransa lapiga maarufuku vazi la "Burqa"

16 Septemba 2010

Ufaransa imekuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kupiga marufuku vazi linalovaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu kufunika viwiliwili vyao, linaloujikana kama Burqa.

https://p.dw.com/p/PE1N
Wanawake waliovaa vazi la Burqa lililopigwa maarufukuPicha: picture alliance/abaca

Masaa machache tu baada ya Bunge la Seneti la nchi hiyo kuiidhinisha rasmi , kukazuka kitisho cha bomu lililotengwa kwenye mnara wa Eifel na kituo cha treni jijini Paris. Makundi ya Waislam wenye msimamo mkali wametishia kufanya mashambulio wakipinga kupigwa marufuku Burqa. Lakini, pamoja na yote, anasema Bernd Riegert, uamuzi huu wa baraza la Seneti la Ufaransa hauhusiani na kuweka vizuizi kwa uhuru wa kuabudu.

Upigaji marufuku wa vazi linalositiri kiwiliwili kizima na uso mzima ulioidhinishwa na Bunge la Ufaransa ni hatua ya haki. Hauna uhusiano wowote na ukosefu wa ustahmilivu au na uhuru wa mtu kufuata dini aitakayo. Vazi linaloziba uso wote, iwe Burqa au Nikab, ni kikwazo kwa maingiliano ya tamaduni, jambo ambalo jamii za Ulaya haziwezi kulistahmilia. Mtu anapokuwa amevaa vazi hili, ni kama kwamba anakusudia kuwaambia watu wengine: "Sitaki kushirikiana nanyi kwa lolote. Hamruhusiwi kuuona uso wangu." Vazi hili si sehemu ya mafunzo ya dini yoyote ile, bali ni mila tu ambayo inatumika kuwapokonya wanawake uhuru na haiba yao. Hoja ya watunga sheria hii ni kwamba, haki ya mtu binafsi kuvaa anavyotaka hapa ni halali.

Ufaransa inakuwa nchi ya mwanzo katika Umoja wa Ulaya kukataza rasmi Burqa na mavazi yanayokifunika kiwiliwili chote na nyuso. Lakini huenda isiwe ya mwisho. Tayari Ubelgiji imo kwenye hatua za awali kuelekea sheria kama hiyo. Nchini Denmark, mvaaji wa mavazi hayo analazimika kujifunua anapokuwa kwenye sehemu za umma. Katika nchi za Uholanzi, Uswisi na Hispania nako suala la upigaji marufuku Burqa linajadiliwa. Italia ina sheria inayofanana na hiyo tangu mwaka 1975. Hata huko Ufaransa, sheria hii haikuwekwa dhidi ya Waislamu tu, bali kwa mwengine yeyote yule. Hii ni kusema ni lazima kila uso wa mtu uonekane. Na hapa Ujerumani pia inawezekana kuwa na mdahalo huu wa mavazi yanayofunika kiwiliwili chote. Kote ambako watu wanataka kuzungumzia haki za wanawake wanaweza kufanya hivyo, na sio juu ya uadui dhidi ya Uislamu.

Tofauti labda iko Uingereza tu, ambako serikali ya vyama vya Conservative na Liberal Democrats hazijaona umuhimu wa kulitia maanani jambo hili.

Mtu hapaswi kuuhusisha mdahalo juu ya mavazi yanayofunika kabisa uso na mdahalo juu ya kuvaa kofia au kilemba. Kwamba tangu hapo mwanzoni, mavazi haya yamekuwa ni alama ya Uislamu kama vile zilivyo alama nyengine kwenye Ukristo. Kutenganisha dini na dola ni katika mafanikio makubwa ya ustaarabu wa Ulaya. Nchini Uturuki kwa kuwa kilemba kilikuwa pia ni alama ya kidini na kisiasa, kilipigwa marufuku kuvaliwa na wanafunzi vyuoni. Lakini hapa Ujerumani, wanafunzi wanaweza kuvaa vilemba vyao mashuleni au vyuoni, jambo ambalp linachangia katika maingiliano ya tamaduni.

Kwa hivyo si sawa kuchukulia kwamba kila anayetoa maoni yake kupinga uvaaji wa mavazi yanayoficha kiwiliwili kizima kuwa ni ana chuki dhidi ya Waislamu na wageni au ni Mnazi mamboleo. Maana, tangu hapo, si kweli kwamba mavazi haya yanaungwa mkono na Waislamu wote.

Badala yake, mdahalo huu katika nchi nyingi za Ulaya unaonesha kuwa wale wanaopinga mavazi haya ni wengi zaidi, kwani uvaaji wake unazidi kuzitenga mbali jamii za Kiislamu na wageni katika mfumo wa maisha ya Ulaya.

Mwandsihi: Riegert, Bernd/Khelef, Mohammed /ZR

Mhariri: Miraji Othman