Bunge la Ufaransa kuamua juu ya mageuzi ya mfumo wa pensheni
16 Machi 2023Suala la utata katika mpango huo ni juu ya kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64. Pamoja na hayo muda wa kuchangia katika mfuko wa mafao utaongezwa na kiwango cha chini cha malipo ya mafao hayo pia kitaongezwa na kufikia Euro 1,200 kwa mwezi.
Mageuzi hayo yanazingatiwa kuwa mpango muhimu wa Rais Emmanuel Macron unaotokana na kutambua hatari ya kukabiliwa na nakisi kwenye mfuko wa pensheni endapo mageuzi yanayokusudiwa na serikali yake hayatafanyika.
Hata hivyo mpango huo unapingwa na vyama vya wafanyakazi na vyama vya wapinzani. Hapo jana maalfu ya wananchi wa Ufaransa walifanya maandamano makubwa kuupinga mpango huo wa mageuzi.
Rais Macron anategemea kura za wabunge wa chama cha Republican ili mpango wake upite bungeni, ingawa wabunge hao wamegawika.