Bunge la shirikisho na baraza la wawakilishi wa majimbo yaidhinisha msaada wa Ujerumani kwa Ugiriki
7 Mei 2010Bunge la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani-Bundestag limeidhinisha mpango wa msaada wa fedha wa Ujerumani kuiokoa Ugiriki- mpango uliopitishwa wiki iliyopita na nchi wanachama wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro pamoja na shirika la fedha la kimataifa, IMF.
Katika bunge la shirikisho, Bundestag, mpango huo ulipitishwa tangu asubuhi kwa sauti 390 dhidi ya 72. Wabunge 139 wa kutoka chama cha upinzani cha Social Democratic, SPD, hawakupiga kura. Baadae ikawa zamu ya baraza la wawakilishi wa majimbo kuupitisha mpango huo.
Rais wa shirikisho, Horst Köhler, anabidi sasa atie saini yake ili mpango huo ukubalike kisheria.
"Uamuzi wa kuidhinisha mpango huo unaonyesha wazi nia ya Ujerumani ya kuhifadhi sarafu ya Euro"- amesema kansela Angela Merkel na kusisitiza tunanukuu: "mataifa yote ya eneo la Euro yanabidi pia kuwajibika," mwisho wa kumnukuu.
Upande wa upinzani unamlaumu kansela kwa kusita sita hapo awali kuhusu mpango huo wa kuisaidia Ugiriki. Mkuu wa kundi la walinzi wa mazingira katika bunge la shirikisho- Bundestag- bibi Renate Künast anasema:
"Kusita sita kwako ndio sababu ya kuongezeka kiwango cha msaada huo, kwetu sisi na kwa Wagiriki pia. Hata kiongozi wa shirika la fedha la kimataifa, Dominique Strauss Kahn, amekua akisema hivyo hivyo mikutanoni. Kitisho ni kikubwa zaidi hivi sasa."
Msaada wa Ugiriki una thamani jumla ya Euro bilioni 110- Euro bilioni 80 kati ya hizo kutoka nchi zinazotumia Euro, bilioni 30 kutoka shirika la fedha la kimataifa, IMF.
Mpango huo utaidhinishwa rasmi wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zinazotumia Euro baadae hii leo mjini Brussels.
Mchango wa Ujerumani unafikia Euro bilioni 22 nukta nne. Wasomi watano wametuma malalamiko yao katika korti kuu ya katiba mjini Karlsruhe dhidi ya mpango huo. Haijulikani, lakini, itachukua muda gani hadi madai yao yatakapochunguzwa.
Miongoni mwao anakutikana Joachim Starbatty, mtaalam wa masuala ya kiuchumi ambae hapendezewi na Umoja wa Ulaya. Wanne wengine waliwahi kushindwa walipotuma malalamiko yao katika mahakama ya katiba mjini Karlsruhe dhidi ya kuanzishwa sarafu ya Euro.
Nchini Ujerumani suala la kupatiwa msaada Ugiriki limehodhi kampeni za uchaguzi utakaofanyika jumapili ijayo katika jimbo la North Rhine Westphalia.
Hisia za wananchi kuelekea msaada huo ndio sababu ya kusita sita kansela Angela Merkel na kupendekeza mpango wa hatua kali za kufunga mikaja.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir /AFP/DPA/Reuter
Imepitiwa na: Miraji Othman