1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPeru

Bunge la Peru lamwapisha Rais mpya Dina Boluarte

Sylvia Mwehozi
8 Desemba 2022

Bunge la Peru limemwapisha Rais mpya Dina Boluarte baada ya kushuhudiwa mabadiliko ya kisiasa kufuatia Rais aliyekuwepo madarakani Pedro Castillo kukamatwa siku ya Jumatano.

https://p.dw.com/p/4KeI2
Peru I Vereidigung der peruanischen Vizepräsidentin Boluarte
Picha: Sebastian Castaneda/REUTERS

Rais wa mrengo wa kushoto Pedro Castillo aliondolewa madarakani na wabunge na kukamatwa siku ya Jumatano baada ya kujaribu kulivunga bunge katika taifa hilo la Amerika ya Kusini katika hatua ambayo imekosolewa kuwa jaribio la mapinduzi.

Wakipuuzia tangazo lake wabunge wa Peru waliendelea na mipango ya awali ya kupiga kura ya kumwondoa madarakani ambapo kura 101 ziliunga mkono rais huyo kuondolewa madarakani na kura 6 za hapana. 

Soma pia: Peru yapata rais mpya wa tatu ndani ya wiki

Matokeo hayo yalipokelewa kwa vifijo bungeni na kisha kumwita makamu wa rais Dina Boluarte kuchukua hatamu. Dina mwenye umri wa miaka 60 amekuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa urais nchini Peru na ataliongza taifa hilo hadi mwaka 2026.

Mara baada ya kuapishwa rais huyo mwanamke ambaye mwaka mmoja uliopita hakuwa anajulikana sana katika ulingo wa siasa za Peru, ametoa wito wa mwafaka wa kisiasa baada ya miezi kadhaa ya kukosekana utulivu ambao umeshuhudia majaribio mawili ya kumwondoa rais mamlakani.

Pedro Castillo | Präsident von Peru
Rais Pedro Castillo aliyeondolewa madarakani PeruPicha: Presidencia Peru/dpa/picture alliance

"Ninachukua madaraka kama rais wa kikatiba wa Jamhuri, nikifahamu wajibu mkubwa unaoniangukia. Na wito wangu wa kwanza, kwani isingeweza kufanyika vinginevyo ni kutoa wito wa umoja mpana zaidi kwa Waperu wote."

Mtafaruku wa kisaisa ulianza jana baada ya Castillo kutangaza kupitia hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya Televisheni kwamba analivunga bunge linalodhibitiwa na upinzani, akianzisha marufuku na kwamba atatawala kwa amri kwa karibu miezi tisa.

Hata hivyo tangazo hilo halikuwazuia wabunge waliokusanyika mapema kuliko ilivyokuwa imepangwa awali kwa ajili ya kupiga kura ya kumwondoa madarakani. Soma pia: Mtoto wa mkulima atangazwa mshindi wa urais Peru

Castillo alilazimika kuondoka Ikulu ya rais akiwa na dhamira ya kuomba hifadhi katika ubalozi wa Mexico kabla ya kukamatwa kwa mujibu wa ripoti ya polisi.

Peru Lima gestürzte Präsident Pedro Castillo von Polizei eskortiert
Rais Castillo baada ya kukamatwa na polisi Picha: Renato Pajuelo/AP/picture alliance

Duru katika ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali zinasema kwamba rais huyo anachunguzwa kwa "uasi". Mwanasiasa huyo amepelekwa katika kituo cha polisi mashariki mwa Lima ambako rais wa zamani wa taifa hilo Alberto Fujimori ambaye pia aliondolewa madarakani na bunge anatumikia kifungo kwa makosa ya ubadhirifu wa fedha.

Mamia ya waandamanaji wanaomuunga mkono na kumpinga Castillo walikusanyika mbele ya majengo ya bunge jana Jumatano.

Kuelekea kura ya kumwondoa madarakani, Marekani ilimtaka Castillo kufuta uamuzi wake na kusema kwamba baada ya kura hiyo haimtambui tena kama rais. Serikali za mataifa ya America Kusini zimeelezea wasiwasi mkubwa na kutoa wito wa kuheshimu demokrasia.