Bunge la Myanmar linamchagua rais mpya
10 Machi 2016Wengi nchini Myanmar walikuwa na matumaini kwamba Bibi Suu Kyi mwenye umri wa miaka 70 na mtu aliyepigania kwa nguvu zote utawala wa kidemokrasi katika taifa hilo lililotawaliwa kwa miaka mingi na wanajeshi, angekuwa mgombea, baada ya ushindi wa kishindo wa chama chake National League for Democracy-NLD katika uchaguzi mkuu mwezi Novemba mwaka jana.
Mwanauchumi Htin Kyaw mwenye umri wa miaka 69 ambaye sasa anamsaidia Bibi Suu Kyi kuongoza wakfu wa misaada na ambaye wakati mmoja alikuwa dereva wake, ameteuliwa kuwa mmoja wapo wa wagombea wawili wa chama hicho katika kinyaganyiro cha Urais, na anatarajiwa na wengi kuwa ndiye atakayechukuwa hatamu za uongozi. Uteuzi wake umekaribishwa na waangalizi na unakuja baada ya miezi kadhaa ya uvumi mkubwa. Mgombea mwengine wa NLD ni mwanasheria na mbunge Henry Van Theu, ambaye atakuwa badala yake Makamu wa rais. Jumla ya wagombea watatu wanawania kiti hicho cha Urais na kwanza watapigiwa kura na wajumbe wa bunge na baadae baraza wajumbe wa kijeshi wanaodhibiti robo tatu ya bunge. Baadae kura ya mwisho itawajumuisha kwa pamoja wajumbe wa vyombo vyote hivyo viwili ambamo NLD ina wingi, na kuamuwa nani awe rais mpya.
Serikali ya kwanza ya kiraia nchini Myanmar
Serikali ya kwanza ya kiraia nchini Myanmar baada ya miongo kadhaa inakabiliwa na changamoto kubwa katika taifa hilo la wakaazi milioni 51 wenye kiu cha kuona kunapatikana mabadiliko baada ya utawala wa kimabavu wa kijeshi na kutengwa kimataifa. Taarifa ya Suu Kyi katika mtandao wa chama chake ilisema, " Hii ni hatua muhimu katika kutekeleza matakwa na matarajio ya wapiga kura ambao kwa shauku kubwa walikiunga mkono chama cha NLD."
Suu Kyi anazuiwa kuwa rais na kifungu cha katiba kwa sababu ya kuwa na watoto aliozaa na mgeni. Mume wa mwanasiasa huyo ambaye sasa ni marehemu alikuwa Muingereza na walizaa watoto wawili wa kiume. Bado Suu Kyi hakufafanua jukumu lake litakuwa lipi, au jinsi atakavyoratibu uongozi wa taifa hilo. Baadhi wanashirai huenda akawa ndiye mwenye usemi serikalini sawa na Bibi Sonia Ghandi nchini India ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa wakati chama chake cha Congress kilipokuwa madarakani. Kumekuweko na fununu kwamba huenda Suu Kyi akawa waziri wa mambo ya nchi za nje, wadhifa ambao pia utamfanya kuwa mjumbe katika Baraza la Usalama wa taifa linalodhibitiwa na wanajeshi.
Majenerali wa zamani walioutawala Myanmar walimuweka Suu Kyi katika kifungo cha nyumbani kwa miaka 15 na hata kufuta ushindi m kubwa wa uchaguzi wa chama chake cha NLD.
Changamoto zitakazoikabili serikali mpya ya kiraia ya kidemokrasi ni pamoja na sekta zilizopuuzwa kwa muda mrefu za afya, elimu na miundo mbinu pamoja na kuondoa tatizo sugu la urasimu. Mwanasiasa huyo ameahidi chama chake kitaunda serikali ya upatanishi wa kitaifa na baraza la mawaziri linatarajiwa kuwashirikisha pia wajumbe kutoka vyama vyengine vya kisiasa.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp
Mhariri:Josephat Charo