Bunge la Marekani lataka msaada wa Marekani kusitishwa Yemen
14 Februari 2019Hatua hiyo ni ya imechukuliwa wakati wabunge wengi wakitaka kumlazimisha rais Donald Trump kuimarisha sera zake kuelekea nchi hiyo ya Kifalme.
Ilikuwa mara ya kwanza baraza hilo la wawakilishi kuunga mkono azimio la madaraka ya vita, lakini kura hiyo iliyoungwa mkono na wabunge 248 kwa 177 waliopinga, kwa karibu kwa misingi ya kichama, haitatosha, hata hivyo, kuweza kuikiuka ahadi ya Trump kutoa kile ambacho kinaweza kuwa kura yake ya kwanza ya turufu.
Ni wabunge 18 tu wa chama cha Trump cha Republican katika baraza hilo la wawakilishi waliojiunga na Wademokrati 230 kuunga mkono azimio linalotaka kuzuwia jeshi la Marekani kujiingiza katika uhasama ndani ama inayoiathiri Yemen, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kujaza mafuta katika ndege zinazofanya mashambulizi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen, bila ya idhini kutoka katika bunge la Marekani Congress.
Wademokrati na Warepublikani walilirejesha tena azimio la madaraka ya kivita wiki mbili zilizopita kama njia ya kutuma ujumbe mzito kwa utawala wa Riyadh juu ya maafa ya kiutu nchini Yemen na kushutumu mauaji ya mwandishi habari wa Saudia, Jamal Khashoggi.
Vita vimewafikisha watu katika ukingo wa njaa
Vita vya Yemen vilivyodumu kwa zaidi ya miaka minne vimewauwa mamia kwa maelfu ya watu, kuvuruga uchumi wa nchi hiyo na kuwafikisha mamilioni ya watu katika ukingo wa kufa njaa.
Utawala huo pamoja na wengi wa wabunge wa chama cha Trump cha Republikani katika baraza la Congress, wamesema azimio hilo halistahili kwa sababu majeshi ya Marekani yamekuwa yakitoa msaada wa kutia mafuta ndege na misaada mingine katika mzozo wa Yemen, na sio wanajeshi. Pia utawala huo umesema hatua hiyo itaathiri uhusiano katika eneo hilo na kuathiri uwezo wa Marekani kuzuwia kuenea kwa ghasia zinazosababishwa na makundi ya itikadi kali.
Baraza la Seneti linatarajiwa kulipigia kura azimio hilo katika muda wa siku 30 zijazo.
Azimio kama hilo la hapo kabla lilipita katika baraza la Seneti kwa kura 56 dhidi ya 41 mwezi Desemba. Lakini azimio hilo halikufikishwa katika baraza la wawakilishi , ambako Warepublican walikuwa na wingi hadi Wademokrati walioshika udhibiti Januari 3 mwaka huu, kufuatia ushindi mkubwa waliopata katika uchaguzi wa mwezi Novemba.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo